Saa saba za JPM, wafanyabiashara

Muktasari:

  • Pamoja na mambo mengine, wadau hao walitaja changamoto ambazo walisema endapo hazitafanyiwa kazi, zitakwamisha juhudi za Serikali za kujenga uchumi wa viwanda.

Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Rais John Magufuli jana alitumia wastani wa saa saba kupokea na kujibu changamoto mbalimbali zilizowasilishwa na wafanyabiashara nchini.

Pamoja na mambo mengine, wadau hao walitaja changamoto ambazo walisema endapo hazitafanyiwa kazi, zitakwamisha juhudi za Serikali za kujenga uchumi wa viwanda.

Katika mkutano huo, baadhi ya hoja mbalimbali zikiwa za kisekta zilijitokeza.

Sekta ya viwanda

Akizungumzia viwanda, Chacha Mwita kutoka Geita aliomba kupunguzwa kodi ya uagizaji wa malighafi za chuma pamoja na kudhibiti bidhaa hafifu na za bei ya chini zinazozalishwa ndani hatua inayoathiri ushindani wa soko la mabati yaliyozalishwa kwa mtaji mkubwa.

Mmiliki wa kiwanda cha kusindika na kuzalisha mafuta ya alizeti cha Mount Meru Millers, Singida, Atul Mittal alisema kasi ya Rais katika kuelekea uchumi wa viwanda inaweza kukwamishwa na wasaidizi wake, akimuomba alinde soko la ndani.

Usafirishaji

Katika sekta ya usafirishaji, Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (Tatoa), Angelina Ngalula aliiomba Serikali iangalie upya uwezekano wa malori ya ndani kutoa huduma katika usambazaji wa mizigo inayoingia bandarini kwa ajili ya soko la ndani.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk Charles Kimei aliomba Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) iendelee kuingiza taarifa za mali za wateja.

Alisema benki haiwezi kukopesha bila kuwa na taarifa za kampuni kutoka Brela.

Ripoti ya sukari

Baada ya kuibuliwa kwa changamoto hizo, Rais Magufuli naye alitoa ripoti ya uchunguzi kuhusu viwanda vya sukari akisema kamati yake imebaini kuwapo viwanda hewa vilivyokuwa vinaagiza sukari ya viwandani.

Alisema Machi 14, alipokea ripoti hiyo na kwamba ni viwanda vinane tu vilivyobainika kuwa na taarifa za kweli za uagizaji wa sukari.

“Viwanda vilivyokuwa vinaagiza industrial sugar kihalali ni viwanda vinane tu, viwanda vingine 22 vimebainika kuwa na dosari ndogondogo, vinaagiza kuliko mahitaji yake... mfano kuna kiwanda ambacho bado hakijakamilika lakini kimeagiza tani 500,000, kumbe kuna viwanda hewa, nilikuwa najua kuna wafanyakazi hewa tu,” alisema.

Aliwataka mawaziri kuandika maelezo yenye majibu ya changamoto na maoni hayo na kuyawasilisha kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ndani ya kipindi cha wiki moja ili Serikali ifanyie kazi na kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji hapa nchini.