Saba washikiliwa kuzama kwa kivuko

Muktasari:

  • Fedha zilizochangwa na watu binafsi, kampuni,taasisi, na mashirika hadi jana jioni ni zaidi ya Sh 589.3 million

Ukerewe/Dar. Watu saba wakiwamo viongozi wa Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa) wanashikiliwa na polisi kwa mahojiano kuhusiana na tukio la kuzama kwa kivuko cha Mv Nyerere.

Akizungumza na Mwananchi jana katika Kijiji cha Bwisya, Ukara ambako operesheni ya uokoaji inafanyika, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jonathan Shanna alisema, “Vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea kutekeleza maagizo kuhusu kuchunguza kwa makini suala hili. Hadi sasa nadhani idadi ya wanaohojiwa imefika saba,” alisema bila kutaja majina ya watuhumiwa kwa sababu za kiuchunguzi

Akiwa Bwisya juzi, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitangaza kushikiliwa kwa mahojiano baadhi ya watendaji na watumishi wa Temesa ili kusaidia uchunguzi wa ajali hiyo ambayo hadi jana imesababisha vifo 227 huku watu 41 wakiokolewa.

“Kama uchunguzi utabaini walihusika kwa namna yoyote hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao,” alisema Majaliwa.

Pamoja na kushikiliwa kwa watendaji hao, Waziri Mkuu pia alitangaza kusimamishwa kazi kwa Mtendaji Mkuu wa Temesa, Musa Mgwatu kupisha uchunguzi wa tume maalumu inayoongozwa na Mkuu wa Majeshi mstaafu, Jenerali George Waitara.

Taarifa zilizolifikia gazeti hili zinaeleza kuwa pamoja na maofisa na watendaji wa Temesa, wengine watakaohojiwa ni baadhi ya maofisa na watendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) wa mkoani Mwanza, Wilaya ya Ukerewe.

Miongoni mwa yanayochunguzwa ni taarifa za usalama na kiufundi za kivuko kabla na wakati wa safari siku kilipozama, mchana wa Septemba 20.

“Utaratibu wa kukata tiketi na kuweka kumbukumbu kwa kuandika orodha ya wasafiri pia ni kati ya yanayochunguzwa iwapo yalikuwa yakizingatiwa,” alisema mmoja wa mtoa taarifa kwa sharti la kuhifadhiwa jina.

Wafiwa wapewa Sh1 milioni

Watu 137 waliopoteza ndugu katika ajali hiyo jana asubuhi walianza kupokea mkono wa pole wa Sh1 milioni kwa kila marehemu aliyetambuliwa.

Awali, ndugu hao walishakabidhiwa mkono wa pole wa Sh500,000 kwa kila mwili uliotambuliwa, hivyo kuongezewa kiasi kingine kama hicho.

Nyongeza ya Sh1 milioni ni agizo la Rais John Magufuli alilolitoa juzi akitaka fedha zote za rambirambi zinazochangwa na mashirika, taasisi, kampuni na watu binafsi kupewa wafiwa.

Fedha hizo pia zitatumika kujenga uzio na makaburi wanakozikwa baadhi ya waliokufa kwenye ajali hiyo iliyotokea Alhamisi Septemba 20.

Huduma za usafiri yarejea

Hayo yakiendelea, huduma ya usafirisha wa abiria na mizigo kutoka na kwenda Ukara itarejea katika hali ya kawaida kuanzia leo.

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Isaac Kamwelwe alisema jana kuwa huduma hiyo itatolewa na kivuko cha Mv Temesa.

“Serikali inatekeleza mipango mahususi ya dharura kuhakikisha wakazi wa Kisiwa cha Ukara wanapata huduma ya usafiri kwa kuagiza mafundi kukifanyia uchunguzi wa kitaalamu kivuko cha Mv Temesa na kukileta Ukara kitoe huduma. Usafiri kati ya Ukara na Bugolora utarejea Jumatano (leo),” alisema.

Alisema kivuko hicho chenye uwezo wa kubeba abiria 120, kitatoa huduma hadi hapo ujenzi wa meli mpya ya tani 50 ambayo Rais Magufuli ameagiza tenda yake itangazwe utakapokamilika.

Tangu kuzama kwa Mv Nyerere, wananchi wanaosafiri kati ya Ukara na Bugolora wanategemea meli binafsi ya Mv Nyehunge inayotumika kusafirisha vifaa, zana, magari, mitambo, wataalamu, maofisa na viongozi mbalimbali wanaofika Ukara kutoa pole, kukagua au kushiriki operesheni ya uokoaji.

Meli hiyo pia ndio hutumika kusafirisha miili ya waliokufa katika ajali hiyo inayochukuliwa na ndugu kwa mazishi nje ya eneo hilo.

Hadi kufikia jana jioni, miili ya watu 227 waliokufa katika ajali hiyo ilikuwa imeopolewa huku watu 41 wakiokolewa wakiwa hai akiwamo fundi mkuu wa kivuko cha Mv Nyerere, Alphonse Charahari aliyeokolewa karibu saa 48 tangu kilipozama.

Operesheni ya kukiinua

Jana, Mkuu wa Majeshi na Ulinzi, Venance Mabeyo alisema baadhi ya milango iliyokuwa imejifunga katika kivuko cha Mv Nyerere imechangia kuchelewesha kazi ya kukiinua ili kiwe katika hali yake ya kawaida.

Akitoa taarifa ya maendeleo ya kuinuliwa kwa kivuko hicho, Jenerali Mabeyo alisema hadi kufikia leo, kazi hiyo itakuwa imekamilika.

“Kwa sababu milango ilikuwa imefungwa hatukutaka kuiharibu, hivyo tulilazimika kuifungua kwa ufanisi ili kupitisha mipira hiyo ambayo tutaijaza upepo ili zoezi liweze kuendelea,” alisema.