Sababu tatu za wenye VVU 19,000 ‘kutoweka’ Temeke

Muktasari:

Takwimu hizo zilizotolewa na Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (Nacopha) ni kutokana na ufuatiliaji katika vituo vya afya vinavyotoa huduma za afya na Ukimwi katika wilaya hiyo.

Dar es Salaam. Sababu tatu zimetajwa kufuatia watu zaidi ya 9,000 wanaoishi na virusi vya Ukimwi kuacha kutumia dawa za kufubaza makali ya ugonjwa huo wilayani Temeke.

Takwimu hizo zilizotolewa na Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (Nacopha) ni kutokana na ufuatiliaji katika vituo vya afya vinavyotoa huduma za afya na Ukimwi katika wilaya hiyo.

Mwenyekiti wa Nacopha wilayani humo, Peter Kisima alisema jana kuwa, sababu zilizobainika kuwaathiri watu hao kufika vituoni ni kukaa katika foleni ya kusubiri huduma kwa muda mrefu, kutetereka kiuchumi baadhi yao na umbali mrefu kati ya vilipo vituo hivyo na sehemu wanazoishi.

Kwa kawaida mtu anayeishi na VVU akiacha kutumia dawa huweza kuambukiza wengine kwa urahisi, virusi kupata nguvu na magonjwa nyemelezi hujitokeza kwa kasi.

“Matibabu ni changamoto kubwa kwetu ukiachilia kupata dawa za kufubaza makali ya VVU ambazo tunapewa bure, tunasumbuliwa sana na maradhi ya hapa na pale,” alisema.

“Kama tutalipiwa bima ya afya itatusaidia kutulia kiakili kwa sababu tutakuwa na uhakika wa matibabu wakati wote. ”

Kauli hiyo ya Kisima imekuja siku chache baada ya Serikali ya Marekani kupitia Mpango wa Dharura wa Rais wa nchi hiyo wa Kukabiliana na Ukimwi (Pepfar), kuidhinisha Dola526 milioni za Marekani kwa ajili ya kukabiliana na VVU na Ukimwi hapa nchini.

Taarifa kuhusu msaada huo zinaeleza kuwa utaongeza idadi ya wanaopata matibabu ya kupunguza makali ya VVU kufikia milioni 1.2.

Pia, msaada huo utaimarisha mapambano dhidi ya VVU kupitia huduma za upimaji, matibabu, kufubaza na kuzuia maambukizi ili hatimaye kufikia lengo la kutokomeza Ukimwi ifikapo mwaka 2030.

Akizungumzia watu 19,000 walioacha dawa, Kisima alisema wanafuatiliwa kwa karibu kutokana na takwimu zinazochukuliwa kila wiki katika vituo vinavyotoa huduma kwa wenye VVU.

“Lakini sisi tunachukua takwimu hizo na baada ya kujua tunawafuatilia kujua kilichowafanya kuacha dawa na tunaendelea kufuatilia,” alisema

Kisima alisema kama fedha za kupambana na VVU zipo, ni vyema pia zikawekezwa kuhakikisha wanaoishi na virusi vya ugonjwa huo wanapata tiba stahiki wakati wote.

Kuhusu changamoto ya kukaa siku nzima kwenye foleni ya kliniki na kuchukua dawa hospitalini, alisema unapaswa uangaliwe utaratibu wa kuwa na vituo vya huduma hiyo kwenye kila kata.

Awali, akizindua ofisi ya Nacopha, tawi la Temeke, Kisima alisema wanaoishi na VVU wanatakiwa kupata ruzuku ili iwasaidie kujikimu na kupata tiba nzuri.

Alisema baadhi ya taasisi za umma zilianzisha utaratibu wa kuwapa posho watumishi wa umma wanaoishi na VVU.

Kisima alisema posho hiyo ilikuwa ikilenga kuwawezesha kununua chakula cha lishe na huduma za afya na kwamba, utaratibu huo unatokana na waraka wa watumishi wa umma namba 2 wa mwaka 2006 kuhusu huduma kwa watumishi wanaoishi na virusi vya Ukimwi na wenye Ukimwi.

Mwenyekiti huyo alisema watu wenye virusi vya Ukimwi (Waviu) wanatakiwa wote kupewa posho hiyo, lakini ni vyema zaidi ikatumika kuwatengenezea bima ya afya ili wasipate shida kupata matibabu.

Kuhusu ujenzi wa ofisi ya Nacopha Temeke, Katibu wa baraza hilo wilaya humo, Baitani Japhes alisema kupatikana kwa eneo katika Mtaa wa Mwembeyanga kutasaidia kupeana taarifa na kuwafikia Waviu kwa ukaribu.

Alisema imo ndani ya ofisi za Serikali ya mtaa na imepatikana kutokana na mradi unaoendelea wa “Sauti Yetu”.

“Konga (baraza la wilaya la Waviu) hii ina vikundi 58 vya ujasiriamali na vicoba na watu 1,260 wanaoishi na VVU ambao sasa watapata taarifa bila usumbufu ule wa awali kabla hatujapata na ofisi,” alisema Japhes.

Alifafanua kuwa ofisi hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kufikia malengo ya 90,90,90, ifikapo mwaka 2030. “Hizi 90 tatu maana yake mafanikio kwa asilimia 90 ya watu kupima na kutambua afya zao, asilimia 90 ya kuanza kutumia dawa kwa usahihi na 90 ya tatu ni kupunguza idadi ya virusi mwilini. ”alifafanua.