VIDEO: Safari ngumu katika vita dhidi ya maradhi yasiyoambukiza

Muktasari:

Maradhi hayo ni yale yasiyoambukiza kama kisukari, saratani, matatizo ya moyo na yale sugu yanayoathiri mfumo wa upumuaji.

Dar es Salaam. Ni zaidi ya miaka minane sasa tangu Shirika la Afya Duniani (WHO) lilipoonya kuwa ifikapo mwaka 2030 watu 52 milioni duniani watafariki kutokana na maradhi yatokanayo na mtindo wa maisha (NCDs).

Maradhi hayo ni yale yasiyoambukiza kama kisukari, saratani, matatizo ya moyo na yale sugu yanayoathiri mfumo wa upumuaji.

Hata hivyo, maradhi hayo yanaendelea kuongezeka.

Tanzania ilianza kampeni dhidi ya maradhi hayo miaka miwili iliyopita, lakini bado haijawa na mafanikio makubwa kwa kuwa juhudi hizo zinategemea utayari wa watu kushiriki kikamilifu katika kampeni hii na kwa kiasi gani wanapata taarifa kuhusu kujikinga na maradhi hayo.

Awali, katika ripoti yake ya kwanza kuhusu maradhi yasiyoambukiza (Global Status Report on Non Communicable Diseases), WHO ilisema kiwango cha magonjwa hayo kitaongezeka katika nchi zenye uchumi wa chini na wa kati ifikapo mwaka 2010.

Hivi karibuni, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema katika mahojiano na Mwananchi kuwa Tanzania imeshaunda sera zote dhidi ya magonjwa hayo. Lakini akasema changamoto ambayo wizara inakabiliana nayo ni namna ya kuhamasisha wananchi wengi kadri iwezekanavyo.

Wakati Waziri Mwalimu akisema hayo, nchi imebakiza miaka miwili tu ya kutimiza malengo hayo (2016-2020), kwa mujibu wa Mpango wa Pili wa Kitaifa wa Kuzuia na Kudhibiti (NCD).

Mpango huo umekuja kutokana na ongezeko la maradhi haya yatokanayo na mtindo wa maisha.

Inakadiriwa yanachangia asilimia 27 ya vifo nchini.

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan alizindua mpango wa ufanyaji mazoezi ya viungo miaka miwili iliyopita, kwa ajili ya kuwahimiza Watanzania wote kujenga utaratibu wa kufanya mazoezi mara kwa mara.

Nia ilikuwa kudhibiti maradhi yasiyoambukiza kwa kauli mbiu isemayo “Afya yako Mtaji Wako.”

Matunda ya kampeni bado

Swali ni kama kampeni hiyo imesaidia ili iendelezwe au haijasaidia ili mkakati ubadilishwe.

“Sidhani,” alisema Waziri Mwalimu. “Ni lazima niwe mkweli katika hili, tulianza vizuri lakini hatukufikia malengo. Ninaona katika baadhi ya maeneo ya nchi, viongozi wanaendelea kuhimiza watu (wafanye mazoezi).”

Alisema kuna mwamko wa kufanya mazoezi miongoni mwa mwananchi kuliko ilivyokuwa awali.

Lakini kwa ngazi ya jamii, alisema bado na akashauri ni vyema kubadili mbinu za uhamasishaji.

Mijini, vijijini wote ni waathirika

Ingawa wengi wanaamini kuwa magonjwa yasiyoambukiza huathiri zaidi watu wa mijini kuliko vijijini, hali ni tofauti.

Kwa mujibu wa Dk Elisha Osati, rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), inamini hiyo inatokana na ukweli kwamba wakazi wa vijijini wanashiriki shughuli nyingi za kutumia nguvu kuliko wa mijini.

Lakini tafiti mbalimbali zinaeleza kuwa maradhi yasiyoambukiza yanaongezeka na kuathiri hata maeneo ya vijijini. Ndiyo maana Dk Osati anasema “hakuna aliye salama”.

“Kutafuta ufumbuzi wa maradhi haya kwa sasa, si suala linalopaswa kutatuliwa hospitalini, tunatakiwa kumfikia kila mmoja, kuanzia kwa wahudumu wa afya hadi kwa wananchi na hospitali iwe ni upimaji,” alisema Dk Osati.

Wengi zaidi hatarini

Utafiti uliofanywa na Serikali mwaka 2012, ulibaini kuwa Watanzania wengi zaidi wanaendelea kuwa katika hatari ya kupata maradhi yasiyoambukiza.

Utafiti huo ulibaini kuwa watumiaji wa tumbaku ni asilimia 15, watumiaji wa pombe, ni asilimia 29.3, wenye unene kupita kiasi asilimia ni 34.4 na wenye lehemu nyingi mwilini ni silimia 26.

Gharama za matibabu

Wakati hayo yakijiri, imeelezwa kuwa ifikapo 2030 gharama za matibabu ya kisukari zitaongezeka na kufikia dola 16.2 bilioni za Kimarekani (takribani Sh40 trilioni), kwa nchi za Tanzania, Kenya na Ethiopia.

Kwa mujibu wa utafiti wa jarida la afya la Lancet, hilo ni ongezeko la dola 3.8 bilioni kwa mwaka 2015.

Kadhalika, Serikali imekuwa ikitumia kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya matibabu ya wagonjwa wa moyo nje ya nchi.

Lakini baada ya kuwekeza kwa kiasi kikubwa kwa kuwafundisha wataalamu wa ndani na kununua vifaatiba na dawa, kwa sasa Tanzania inatumia kiasi kidogo cha fedha kwa matibabu hayo hapa nchini.

Takwimu za Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) zinaonyesha katika kipindi cha kuanzia Julai 2017, idadi ya Watanzania wanaokwenda kutibiwa nje ya nchi kwa matatizo ya moyo imepungua.

Takwimu hizo zinaeleza kuwa, idadi hiyo imepungua kwa asilimia 95.5 kutoka wagonjwa 159 mwaka 2012 hadi wagonjwa wanne tu, mwaka 2016.

Rais wa MAT, Dk Obadia Nyongole anasema hata hivyo wanaoishi na maradhi ya moyo, bado wanatumia gharama kubwa katika matibabu.

“Ni lazima tujikite zaidi katika kuzuia, kuliko kutibu,” anashauri Dk Nyongole.

Hapa nchini kwa sasa, vifo 21,000 vinavyotokana na saratani viliripotiwa mwaka 2014 na kuna wagonjwa wapya 35,000 kila mwaka.

Licha ya kuwa saratani ni miongoni mwa maradhi yanayotishia katika sekta ya afya, nchi ina vituo vichache vya matibabu ya ugonjwa huo.

“Saratani, ikigundulika mapema, inaweza kuondolewa na hili linaweza kuokoa maisha ya mgonjwa na mzigo wa matibabu,” anasema Dk Nyongole.

Dk Nyongole alisema kwamba saratani inahitaji matibabu ya muda mrefu, ndiyo maana inasisitizwa kuwekeza katika kujikinga zaidi badala ya kusubiri kuanza matibabu.

Waswahili husema “usipoziba ufa, utajenga ukuta.”