Safari ya Nangole kurejea mjengoni

Muktasari:

Rufaa hiyo inaanza kusikilizwa leo katika Mahakama ya Rufani, huku hukumu yake ikipangwa kutolewa Februari 23.

Arusha. Baada ya kukaa nje ya Bunge kwa miezi minane kutokana na matokeo ya ushindi wa aliyekuwa Mbunge wa Longido, Onesmo ole Nangole kutenguliwa na Mahakama Kuu, leo anaaza safari ya kuona iwapo Mahakama ya Rufani itamrejesha.

Rufaa hiyo inaanza kusikilizwa leo katika Mahakama ya Rufani, huku hukumu yake ikipangwa kutolewa Februari 23.

Mwaka jana, Mahakama ya Rufani iliahirisha hukumu ya kesi hiyo kwa madai hadi mkurugenzi wa uchaguzi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali watakapojumuishwa kwenye rufaa hiyo.

Msajili wa Mahakama ya Rufani nchini, John Kahyoza akisoma uamuzi huo  mwishoni mwa mwaka jana, alitoa siku 21 kwa upande wa wakata rufaa kurekebisha taarifa yao.

Juni 29, 2016, Jaji Silvangilwa Mwangesi alitengua ubunge wa ole Nangole kutokana na matokeo ya ubunge kujazwa kwenye fomu za udiwani. Katika shauri hilo, aliyekuwa mgombea ubunge wa CCM, Dk Stephen Kiruswa alifikisha mahakamani shauri hilo kupinga matokeo ya ushindi dhidi ya ole Nangole kwa madai kwamba utaratibu wa uchaguzi ulikuwa batili.