VIDEO: Safari ya uchumi wa viwanda yaanza

Muktasari:

Waziri alipendekeza kufuta baadhi ya kodi, tozo na ushuru unaotozwa kwenye biashara, malighafi au sehemu ya matakwa ya kiutawala.

Dar es Salaam. Hatimaye Serikali imewasilisha bajeti inayoonyesha imepania kuhamasisha na kuchochea uchumi wa viwanda kwa kutoongeza kodi au kuondoa za bidhaa zinazozalishwa nchini na kuongeza katika bidhaa zinazoagizwa kutoka nje.

Jana Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango aliwasilisha bajeti ya Serikali yenye dhima inayoendana na nchi nyingine wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ya “kujenga uchumi wa viwanda utakaochochea ajira na ustawi endelevu wa jamii”.

Kufanikisha hilo, waziri alipendekeza kufuta baadhi ya kodi, tozo na ushuru unaotozwa kwenye biashara, malighafi au sehemu ya matakwa ya kiutawala.

Kwenye vipaumbele vitano kwa mwaka ujao wa fedha, waziri alisema Serikali inakusudia kuchochea ukuaji wa viwanda kwa kuboresha mfumo wa udhibiti biashara ili kuvutia uwekezaji hususan viwanda vya nguo, ngozi na nyama.

Viwanda vingine vya kimkakati, Dk Mpango alisema, ni vya kusindika samaki, mafuta ya kula, dawa na vifaa tiba, vyakula na kuchenjua na kuchakata madini.

“Malengo makuu ya bejeti hii ni kuondokana na umaskini na kuibadilisha Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa viwanda yenye kipato cha kati mwaka 2025,” alisema Dk Mpango.

Maeneo mengine ya kipaumbele alisema ni kilimo ambacho alibainisha kuwa fedha zitaelekezwa zaidi kuboresha miundombinu ya umwagiliaji, maghala na masoko.

Huduma za jamii hasa maji, elimu na afya ni kipaumbele kingine kitakachopewa msisitizo mwaka ujao wa fedha.

Serikali pia itajenga na kukarabati miundombinu wezeshi hususan kuongeza uzalishaji wa umeme, kuendelea na ujenzi wa reli mpya ya kati kwa kiwango cha kimataifa (standard gauge), barabara za kuunganisha mikoa na vijijini, na kuimarisha usafiri wa anga na majini.

Maeneo mengine ya kipaumbele alisema ni kurahisisha umiliki wa ardhi, kuimarisha huduma za mawasiliano, fedha na utalii, na kuimarisha ulinzi, usalama, utawala bora, na utoaji haki.

Kodi, tozo zafutwa

Akieleza hatua ambazo Serikali imechukua kuhamasisha uzalishaji wa ndani, waziri alipendekeza kufanya marekebisho yatakayoruhusu kufuta baadhi ya kodi na tozo zilizopo.

Waziri alipendekeza kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye vifungashio vya dawa za binadamu zitakazozalishwa nchini, virutubisho vinavyotumika kutengenezea vyakula vinavyoagizwa kutoka nje na kutoa msamaha kwa miradi inayotekelezwa kwa mikopo ya kibiashara.

Waziri pia alitangaza kusamehe VAT kwenye taulo za kike ili kuwezesha upatikanaji wa bidhaa hiyo muhimu kwa bei nafuu kwa ajili ya kulinda afya ya mama na mtoto wa kike, hasa watoto walio shuleni na vijijini.

Habari hiyo ilisababisha wabunge kulipuka kelele za shangwe kiasi cha kumshawishi Spika Job Ndugai kumtaka waziri arudie tena kuutangaza.

Vilevile, waziri alifanya marekebisho kwenye Sheria ya Kodi ya Mapato na kupunguza Kodi ya Mapato ya Kampuni (Corporate Income Tax) kutoka asilimia 30 mpaka asilimia 20 kwa miaka mitano; kuanzia mwaka 2018/19 hadi 2022/23 kwa wawekezaji wapya wa viwanda vya dawa na bidhaa za ngozi.

Ili kujenga uchumi wa viwanda, waziri hakufanya mabadiliko ya ushuru wa bidhaa zisizo za petroli zinazozalishwa nchini, bali aliongeza kwa zile zinazoagizwa kutoka nje ya nchi.

Alipendekeza kuongeza ushuru wa maji ya kunywa yaliyo kwenye chupa kutoka nje kutoka Sh61 kwa lita hadi Sh64.05, wakati ule wa juisi kutoka nje ukipanda kutoka Sh221 hadi Sh232 kwa lita. Wakati ushuru wa bia za ndani ukiendelea kubaki Sh450, wa vinywaji hivyo vinavyoagizwa kutoka nje umepandishwa kwa Sh38.25 mpaka Sh803.25 kwa lita.

Alipendekeza pia kuongeza Sh174.05 kwenye ushuru wa vinywaji vikali kutoka nje na kufika Sh3,655.05 kwa lita, huku vile vya ndani vikibaki kama vilivyo. Ushuru wa sigara za nje umeongezeka kutoka Sh53,235 hadi Sh55,896.75 kwa kila sigara 1,000.

Waziri pia amependekeza kuanzisha mfumo wa stempu za kodi za kielektroniki utakaoanza kutumika Septemba Mosi, kuanzisha utaratibu maalumu wa kusamehe kabisa malimbikizo ya riba na adhabu ya kodi. Msamaha huo, amesema utatolewa kwa miezi sita kuanzia Julai Mosi hadi Desemba 31.

Serikali pia imeshusha ushuru wa forodha kwenye ngano kutoka asilimia 35 hadi 10 kuvipa unafuu viwanda husika, huku ikiongeza ushuru kwenye sukari ya nyumbani kutoka asilimia 25 hadi 35.