Friday, September 14, 2018

Safari za anga kufanya doria misituni

 

By Elizabeth Edward, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), umeanza kutumia safari za anga kufanya doria kukabiliana na changamoto kubwa inayoikabili Serikali katika uhifadhi wa sekta ya misitu na maliasili.

Akizungumza leo Septemba 14, 2018 mtendaji mkuu wa TFS, Profesa Dos Santos Silayo amesema lengo la doria hizo ni kuhakikisha ulinzi unaimarishwa maeneo yote ya misitu ambayo wakala huo umepewa dhamana ya kuilinda.
“Nimeelekeza watendaji wangu kufanya doria ya anga kuanzia leo na tutaanza na Kanda ya Mashariki na nizitake kanda nyingine zijipange, maeneo korofi yabainiwe na kutafuta ramani zake. Nitawatumia ndege kwa ajili ya doria kutambua uharibifu," amesema Profesa Santos na kuongeza:
“Tumekuwa tukifanya doria za misitu tunapata wakati mgumu kuyafikia maeneo yote, lakini kupitia doria za anga sasa tutajua kila kinachoendelea kwenye eneo la misitu na kwa kutumia vikosi kazi vyetu tutafanya ulinzi kwa uhakika zaidi.”
Naye meneja msaidizi wa TFS Kanda ya Mashariki, Bernadetha Kadala alisema doria hizo zimewawezesha kuona kwa karibu zaidi hali halisi ya misitu iliyopo kwenye kanda hiyo.
Amesema doria hiyo imewezesha  kufahamu kuna nini kinachotokea kwa wakati huo hivyo itawawezesha kufanya ulinzi kwa weledi.

-->