Sahara Energy kuunga mkono sekta ya afya, elimu

Muktasari:

Meneja wa huduma kwa Jamii wa kampuni hiyo, Babatomiwa Adesida amesema kuwa mchango huo utatolewa kupitia utaratibu wa kampuni hiyo wa kutoa sehemu ya faida yake kwa jamii inayoizunguka.

Nigeria. Kampuni ya Sahara Energy imeeleza azma yake ya kuunga mkono juhudi za Serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo katika kutoa mchango wake kwenye sekta za afya na elimu.

Meneja wa huduma kwa Jamii wa kampuni hiyo, Babatomiwa Adesida amesema kuwa mchango huo utatolewa kupitia utaratibu wa kampuni hiyo wa kutoa sehemu ya faida yake kwa jamii inayoizunguka.

Adesida amesema tayari kampuni hiyo ambayo ilisajiliwa na kuanza shughuli zake za uuzaji wa mafuta nchini tangu mwaka 2014, iko kwenye upembuzi yakinifu ili kubaini shule na hospitali zenye mahitaji zaidi kabla ya kuanza utoa mchango wao ifikapo Novemba mwaka huu.

Pia amesema iwapo upembuzi huo utabaini maeneo mengine yenye uhitaji haitasita kutoa mchango wake ili uhakikisha jamii ya Tanzania inanufaika na faida Sahara Energy inayopata kupitia shughuli zake inazofanya nchini.