Sahara Energy yatoa fursa za ajira kwa vijana, wanawake nchini

Wakurugenzi wakuu wa Kampuni ya Sahara Energy ya nchini Nigeria, Tope Shonubi (Kushoto) na Tonye Cole (Kulia). Picha na Suzan Mwillo

Muktasari:

Tope Shonubi na Tonye Cole wamesema mbali na Tanzania ambayo imegundua nishati ya gesi asilia kupata fursa ya kujifunza masuala mbalimbali kuhusu gesi na mafuta, kampuni hiyo inalenga kuhakikisha vijana na wanawake wenye uwezo na juhudi katika kazi wanapewa kipaumbele.

Nigeria. Wakurugenzi wakuu wa Kampuni ya Sahara Energy wamesema tawi la kampuni ni hiyo nchini Tanzania litafungua fursa mbalimbali kwa Tanzania ikiwa ni pamoja na ajira kwa vijana na wanawake.

Tope Shonubi na Tonye Cole wamesema mbali na Tanzania ambayo imegundua nishati ya gesi asilia kupata fursa ya kujifunza masuala mbalimbali kuhusu gesi na mafuta, kampuni hiyo inalenga kuhakikisha vijana na wanawake wenye uwezo na juhudi katika kazi wanapewa kipaumbele.

Wakurugenzi hao ambao pia ni waanzilishi wa kampuni ya Sahara Energy yenye matawi katika baadhi ya nchi duniani, ikiwamo Dubai, Ivory Coast, Geneva na Singapore wamesema waanamini kuwa vijana wana uwezo na ubunifu mkubwa hasa pale wanapopewa fursa za kuonyesha uwezo wao.

Shonubi alisema  wanadhamini utayari wa Tanzania wa kuwafungulia mlango ili waweze kufanya shughuli zao za nchini.

Kutokana na hilo, ameendelea kuishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuwapa nafasi hiyo na kusema kuwa itakuwa kitovu chao cha biashara kwa ajili ya kufikia nchi nyingine za Afrika Mashariki kama Rwanda, Kenya na Uganda.

Mbali na hilo, amesema  Tanzania ina nafasi kubwa ya utumia fursa ya gesi kupiga hatua kubwa ya maendeleo hasa katika kipindi ambacho kimepata Rais (John Magufuli) ambaye tangu alipoingia madarakani ameonyesha kuwa kiongozi anayepingana na rushwa na matumizi mabaya ya madaraka.