Thursday, November 16, 2017

Spika ataka Serikali kutoa majibu kuhusu walimu kukutwa wamelala nje

 

By Habel Chidawali,Mwananchi hchidawali@mwananchi.co.tz

Dodoma. Sakata la walimu saba katika Wilaya ya Sengerema ambao walikutwa wakiwa wamelala nje ya nyumba zao huku baadhi wakiwa wamenyolewa nywele, limetinga bungeni leo Alhamisi.

Spika wa Bunge, Job Ndugai ametaka Serikali kutoa maelezo ya kutosha kuhusu walimu hao na namna walivyonyolewa yeye akisema ‘walinyolewa sehemu zote’.

Leo vyombo vya habari vimeripoti kuhusu walimu wa Shule ya Msingi Soswa iliyopo Buchosa ambao walikutwa na mkasa huo wao na familia zao kitendo kilichohusishwa na imani za kishirikina.

Taarifa iliyomkariri mwalimu wa shule hiyo Petro Lukas ilieleza kuwa walimu hao walilala ndani ya vyumba vyao lakini walipoamka walijikuta wao na familia zao wakiwa nje ya nyumba.

“Mheshimiwa Naibu Waziri kabla hujaondoka mahali hapo naomba utusaidie kutoa ufafanuzi wa kile kilichotokea huko mkoani Mwanza ambako nasikia walimu walijikuta wakiwa nje utupu tena baadhi wakiwa wamenyolewa nywele maeneo mbalimbali hivi kuna ukweli,” ameuliza Spika

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, William Ole Nasha alikiri kuwa taarifa hizo wanazo wizarani lakini akasema Serikali haiamini masuala ya ushirikina ambao unaonekana kuhusishwa katika sakata hilo.

“Mheshimiwa Spika taarifa hizo tunazo, lakini kama mnavyojua Serikali haiamini masuala ya ushirikisha, hata hivyo tumeagiza wenzetu huko kushughulikia jambo hilo kikamilifu na mara tutakapopata taarifa kamili tutasema,” amesema Ole Nasha

Ole Nasha amewataka wananchi kutoa ushirikiana kwa walimu ili wawape nafasi ya kufanya kazi kwa uhuru zaidi kwa ajili ya kuwaelimisha vijana na watoto wa Kitanzania.

 

-->