Sakata la Lissu, Saanane lalichemsha Bunge

Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bunge, Freeman Mbowe (kulia) akimuuliza swali Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika kikao cha tatu cha mkutano wa tisa wa Bunge, mjini Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi

Dodoma. Sakata la kushambuliwa kwa mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, kuuawa kwa mwenyekiti wa chama hicho mkoani Geita, Alphonce Mawazo na kutoweka kwa Ben Saanane jana liliibua tuhuma tofauti baada ya kuibuliwa tena bungeni.

Sakata hilo liliibuliwa na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe aliyetaka kujua sababu za Serikali kuonekana inachelea kufanya uchunguzi na kujibiwa kuwa vyombo vya dola vinalishughulikia kama linavyochunguza mauaji ya viongozi wa vijiji katika wilaya za mkoani Pwani na vitatoa taarifa.

Lakini mbunge wa Ulanga (CCM), Goodluck Mlinga akaomba mwongozo wa Spika, akimtuhumu Mbowe kukiuka Katiba kutokana na kutaka uchunguzi wa nje wa mashambulizi na mauaji hayo, lakini baadaye akakumbana na ombi la mbunge wa Chadema kutaka Mlinga ahusishwe na shambulizi dhidi ya Lissu kwa kuwa alishawahi kuhusishwa kwa mauaji.

‘Sinema’ ilianza kwa Mbowe kumuuliza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuhusu matukio hayo dhidi ya viongozi wa Chadema, akisema Serikali haijachukua hatua yoyote.

Mbowe alihoji hayo katika kipindi cha maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ambaye aliendelea kusisitiza kuwa Serikali inaviamini vyombo vyake vyake vinavyoendelea na uchunguzi na kwamba hakuna haja ya kuita wachunguzi kutoka nje.

“Tukio la kushambuliwa kwa risasi kwa nia ya kuua kwa Mheshimiwa Tundu Lissu limezua hofu kubwa si tu kwa Taifa tu, bali bara zima la Afrika na jumuiya ya kimataifa,” alisema Mbowe.

Alisema baada ya kupotea kwa Saanane, alimuomba Waziri Mkuu aruhusu aombe wachunguzi huru kutoka nje, lakini Serikali inaonekana ina kigugumizi.

Lakini, Majaliwa alisema matukio hayo hayapo kwenye siasa tu bali yapo katika maeneo mengine na yamekuwa yakifanywa na watu wasioitakia mema amani ya Tanzania.

“Hatupendi matukio haya yatokee, lakini pia utakumbuka wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiki tumepoteza watu wengi,” alisema Waziri Mkuu na kusababisha wabunge wachache kumpigia makofi.

“Lakini pia hata siku za karibuni, kamanda wetu wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) naye alipigwa risasi. Kwa hiyo tuyazungumze haya kwa ujumla wake.”

Alilihakikishia Bunge kuwa uchunguzi unaendelea na utachukua muda mrefu kukamilika.

Lakini Mbowe alisema Serikali isipunguze uzito tukio la Lissu kwa kulichanganya na matukio mengine mengi ya uhalifu, akisema wakati Benki Kuu ilipoungua, Scotland Yard walialikwa kufanya uchunguzi hivyo si jambo jipya.

Naye mbunge wa Ulanga (CCM), Goodluck Mlinga aliibua utata baada ya kuomba mwongozo, akidai Mbowe amevunja Katiba kwa kutaka uchunguzi huru wa taasisi za nje.

Alisema Katiba inasema binadamu wote ni sawa na wote wanastahili kuheshimiwa.

“Sasa kwanini Mbowe hakuomba uchunguzi kwenye matukio ya mauaji ya albino, halafu aombe kwa Lissu?” alihoji.

Naye mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini aliomba Mlinga ahusishwe katika uchunguzi wa tukio la kushambuliwa kwa Lissu.

Selasini alisema Mlinga alishahusisha na mauaji ya mpenzi wa mpenzi wake, hivyo ni vyema akahusisha na uchunguzi huo.

Hata hivyo, Mlinga alitoa taarifa kuwa hajawahi kuhusishwa na mauaji.

Hata hivyo, Selasini aliendelea na tuhuma zake.

“Nimemsikia na huo ni mkuki kwa nguruwe lakini kwa binadamu ni mchungu. Gazeti la Dira liliandika vizuri sana kuwa mpenzi wako alikusaliti,”alisema Selasini na kuongeza kusema;-

“Wewe na kundi la vijana wenzako mkaenda kumuua na liliripotiwa polisi na limeripotiwa kwenye magazeti na hujawahi kukanusha hadi leo”

“Na ningeiomba Serikali katika uchunguzi wa nani waliohusika kutaka kudhulumu maisha ya Tundu Lussu, huyu ambaye ameshatajwa kwamba alihusishwa na mauaji uchunguzi uanzie kwake,”alisema.