Sakata la mama aliyedai kuibiwa kichanga Temeke laanza upya


Dar es Salaam. Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu leo ameunda Tume huru aliyoipa siku 14 kwa ajili ya kuchunguza suala la Asma Juma Elias anayelalamika kuibiwa kichanga chake katika Hospitali ya Temeke.

Waziri ameunda tume hiyo leo asubuhi na kuipa siku 14, baada ya Asma kufika ofisini kwake na kukataa majibu ya tume iliyoundwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

"Tume hii itaongozwa na mtaalamu wa magonjwa ya kinamama Profesa Charles Majinge na Muuguzi Mkuu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Agnes Mtawa na wataalamu wengine wakiwemo wa radiolojia," alisema Ummy Mwalimu.