Sakaya, wenzake watinga kortini

Mbunge wa Kaliua Tabora, Magdalena Sakaya

Muktasari:

Ngole kwa niaba ya wateja wake hao wanadai kuwa maombi yaliyowasilishwa mahakamani hapo na bodi ya wadhamini ya CUF kupitia Wakili, Hashimu Mziray hayawezi kusikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Dar es Salaam. Hatimaye mbunge wa Kaliua Tabora, Magdalena Sakaya na wenzake saba kupitia Wakili wao, Mashaka Ngole wamewasilisha pingamizi la awali katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu dhidi ya kesi ya madai iliyofunguliwa na Bodi ya Wadhamini ya Chama cha Wananchi (CUF).

Ngole kwa niaba ya wateja wake hao wanadai kuwa maombi yaliyowasilishwa mahakamani hapo na bodi ya wadhamini ya CUF kupitia Wakili, Hashimu Mziray hayawezi kusikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Ngole alidai kuwa muombaji hana mamlaka ya kufungua kesi dhidi ya wajibu maombi na kwamba, maombi hayo hayana msingi kwa sababu yameshindwa kubainisha jina la mwandishi wa masuala ya fedha.

Wanaiomba mahakama kuyatupilia mbali kwa gharama.

Wakili wa bodi ya wadhamini wa CUF, Mziray aliiambia mahakama kuwa walikwisha patiwa nakala ya pingamizi hilo na hati kinzani na akaomba apatiwe muda wa wa kujibu.

Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbroad Mashauri alipanga Aprili 12, ndiyo pingamizi hilo la awali litasikilizwa mahakamani hapo.