WCB wakanusha ugomvi na Clouds Media

Muktasari:

Posti hizo zinahusishwa na sakata la dansa wa WCB, Moze Iyobo na watangazaji wa kipindi cha Shilawadu.


Dar es Salaam. Mmoja wa mameneja wa Nassib Abdul maarufu kama Diamond Platnumz, Sallam Sharaf amekanusha kuwa na matatizo na uongozi wa Clouds Media Group na kwamba wana ushirikiano mzuri wa kikazi.

Minong’ono ya kuwepo kwa tofauti kati yao ilianza mapema leo Februari 7, 2018 baada ya  mfululizo wa posti katika mtandao wa kijamii wa Instagram unaohusisha pande zote mbili,  wakihusisha tukio la madai ya kushambuliwa kwa watangazaji wa kipindi cha Shilawadu kinachorushwa na televisheni ya Clouds.

Sallam aliandika waraka aliouambatanisha na picha ya Diamond akisema: “Kumbe tatizo ni kumpoteza huyu kijana? Waambie familia yako na wazazi waliokuleta katika haya maisha huyu mtoto kaletwa kwa makusudi maisha haya, ili kuleta ukombozi wa dhuluma uliyokuwa unaleta kwenye Taifa hili, unatikiwa kujua Kwanza hili Taifa sasa Rais anaitwa John Pombe Magufuli.”

Saa sita baadaye dansa wa Diamond, Mose Iyobo aliposti picha akiwa na Diamond na kuandika: Nishapoa simba ila lengo lao ni wewe mie kioo tu.”

Kauli hizo zimewavuta mashabiki mitandaoni waliohusisha kauli hizo na sintofahamu iliyoibuka wiki iliyopita hasa baada ya watangazaji wa Shilawadu kudai kuwa wameshambuliwa na Iyobo, madai ambayo dansa huyo ameyakanusha.

Sallam amesema yanayoendelea ni mambo ya kawaida na hakuna bifu ndiyo maana Clouds televisheni na redio  wanacheza nyimbo za wasanii wa WCB kama kawaida, ameahidi kutoa taarifa rasmi baadaye leo.

“Msiwe na haraka, tutatoa statement (taarifa) muda si mrefu na tutawatumia wote, ”amesema Sallam.