Salumu Mwalimu atoa neno

Muktasari:

Akizungumza na Mwananchi, Msemaji wa Chadema, Tumaini Makene amethibitisha kifo hicho akisema Hiza amefariki leo asubuhi nyumbani kwake Mbagala akiwa amelala.

Dar es Salaam. Kada wa Chadema, Richard Tambwe Hiza amefariki dunia leo asubuhi Februari 8, 2018 kwa ugonjwa wa pumu.

Akizungumza na Mwananchi, Msemaji wa Chadema, Tumaini Makene amethibitisha kifo hicho akisema Hiza amefariki leo asubuhi nyumbani kwake Mbagala akiwa amelala.

Hiza amefariki kipindi ambacho alikuwa katika timu ya kampeni za kumnadi mgombea wa ubunge wa Chama hicho katika Jimbo la Kinondoni, Salumu Mwalimu na jana jioni alipanda jukwaani kumnadi.

Mwalimu akizumzia kifo hicho amesema “sina maneno yanayoweza kumwelezea Tambwe, Tambwe alikuwa mtu muhimu sana katika timu yangu ya kampeni, kaniacha kipindi muhimu sana.”

“Alikuwa nguzo yangu, katika muda aliokuwa nasi ndani ya chama Tambwe alikuwa na ushawishi mkubwa sana, hadi jana saa 4 usiku tulikuwa sote, Tambwe kaniacha kipindi muhimu kweli kweli sijui hata niseme nini,” ameongeza Mwalimu

Kuhusu kuendelea na kampeni, Mwalimu amesema “mimi binafsi sidhani kama nitaweza, lakini ngoja nisubiri chama, kwa sasa nakwenda msibani ila baadae tutajua.”

 

 

Mwaka 2015, Hiza alitangaza kujiunga na Chadema wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu akitokea CCM ambako aliwahi kuhudumu kama mkuu wa kitengo cha propaganda wa chama hicho tawala.

Kabla ya kujiunga na CCM alihama kutoka katika Chama cha Wananchi (CUF) ambako pia alihamia kutoka NCCR-Mageuzi.

Katika kampeni za urais 2-15, Hiza alikuwa katika jopo la kumnadi mgombea wa Chadema aliyeungwa mkono na vyama vinavyounda Ukawa, Edward Lowassa na mara zote alikuwa anapanda jukwaani mwanzoni kama alivyokuwa akifanya kwenye kampeni za  Mwalimu zinazoendelea.