Saluti ya polisi kwa Lipumba gumzo

Askari wa Jeshi la Polisi akimpigia Saluti Mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Profesa Ibrahim Lipumba

Muktasari:

Juzi, Polisi alionekana akimpigia saluti Profesa Lipumba katika eneo la Buguruni alipokwenda kufanya usafi. Kitendo hicho kimeibua mjadala mitandaoni, watu wakihoji uhalali wa mwanasiasa huyo kupewa heshima hiyo.

Dar es Salaam. Suala la polisi kumpigia saluti mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Profesa Ibrahim Lipumba limezua mjadala baada ya kuonekana kuwa si mmoja wa viongozi wanaopaswa kupata heshima hiyo kisheria.

Juzi, Polisi alionekana akimpigia saluti Profesa Lipumba katika eneo la Buguruni alipokwenda kufanya usafi. Kitendo hicho kimeibua mjadala mitandaoni, watu wakihoji uhalali wa mwanasiasa huyo kupewa heshima hiyo.

Juni 2005, aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Kapteni John Chiligati alipokuwa akijibu swali la aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu, Salome Mbatia alibainisha maana ya saluti na makundi ya watu wanaostahili kupigiwa saluti na askari.

Chiligati alisema saluti ni kitendo kinachofanywa na askari kwa maana ya kutoa salamu kwa ishara yenye kuonyesha heshima. Pia, alisema saluti ni njia mojawapo ya kuonyesha heshima na utii kwa kiongozi mkuu kwenye asasi za kijeshi.