Samaki waliovuliwa Msumbiji wapigwa mnada Mtwara

Muktasari:

  • Samaki waliovuliwa Msumbiji na kuingizwa nchini bila kufuata taratibu wamepigwa mnada kutokana na amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Mtwara

Mtwara. Samaki waliovuliwa Msumbiji na kuingizwa nchini bila kufuata taratibu wamepigwa mnada kutokana na amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Mtwara.

 Akizungumza leo Jumatano Septemba 19, 2018 hakimu wa mahakama hiyo, James Muhoni amesema wamelazimika kuwapiga mnada samaki hao kutokana na kushindwa kuwahifadhi  wakati taratibu za kisheria zikiendelea, kwamba wameuzwa Sh5.2 milioni.

 Mwenyekiti wa soko la feri ulipofanyika mnada huo, Mwinyi Mzaina amesema, “mvuvi halali anatakiwa awe na leseni halali na atambulike, lakini hawa wamekamatwa baharini wanafanya shughuli za uvuvi na kusafirisha mali za bahari bila leseni.”

 “Kwa hiyo kisheria hawaruhusiwi ndio maana samaki wamekamatwa na wanapigwa mnada baada ya kufuata taratibu zote, na leo kama wangelala wangeharibika.”

 Amesema, “wavuvi wasitumie njia za mkato, kazi ya uvuvi inatambulika na Serikali kama kazi nyingine, leseni ya uvuvi ni Sh 25,000 lakini hapa tumeona samaki waliotaifishwa wanauzwa hadi Sh 700,000. Nitoe wito kwa wavuvi wafuate masharti yaliyowekwa na serikali kuepuka matatizo mengine.”

 Mchuuzi wa samaki katika soko la Mtwara, Said Kambona amesema samaki hao kuuzwa Mtwara kumewafaidisha kwa sababu watawauza kwa watu mbalimbali.

 Mnada huo umesimamiwa na watendaji wa Serikali kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambao hawakuwa tayari kuzungumza chochote, wakitaka atafutwe Waziri wa wizara hiyo.