Samia atishwa mmomonyoka wa maadili kwa vijana nchini

Muktasari:

Ayataka makanisa kulinda amani na utulivu wa nchi, kujiepusha na migogoro

Kigoma. Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ametishwa na mmomonyoko wa maadili miongoni mwa vijana nchini  kutokana na matumizi mabaya ya maendeleo ya sayansi na teknolojia na kulitaka kanisa kupiga vita hali hiyo badala ya kujihusisha na siasa na migogoro ya kiutawala.

Samia alitoa rai hiyo leo mjini Kigoma katika  ibada ya kuwekwa wakfu kwa Askofu Mkuu Msaidizi wa Pentekosti ya Motomoto ya kanisa la PMC na maaskofu wengine wanne wa kanisa hilo.

Alisema Serikali inalitegemea kanisa katika kujenga maadili mema kwenye jamii, hasa kwa kuzingatiwa kuwa miaka ya hivi karibuni Taifa limeshuhudia mmomonyoko mkubwa wa maadili katika jamii kutokana na matumizi mabaya ya maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Alisema hali hiyo imetoa nafasi kwa vijana kuiga tamaduni za kigeni, baadhi zikiwa na mambo yasiyokubalika katika jamii ya Watanzania.

“Ni matumaini yangu kuwa kanisa litaendelea kusaidiana na serikali katika kupiga vita tamaduni mbaya za nje ili kujenga Taifa lenye maadili ya Kitanzania,” alisema.

Aidha, Makamu wa Rais alisema kanisa linajukumu la kuhubiri amani kwa waumini wake na kuyataka kujiepusha na migogoro ya kiutawala.

Alisema makanisa yanapaswa kuhubiri amani na kwamba Serikali haipendi kuona migogoro ndani ya nyumba za ibada.

 “Katika kuhakikisha kanisa linalinda amani na utulivu wa nchi yetu ni lazima lijiepushe na migogoro ya kiutawala na pia kujiepusha kuchanganya dini na siasa," alisema.

Katika ibada hiyo maaskofu waliowekwa wakfu ni Askofu Mkuu Msaidizi, Bwami Mathias, Askofu wa Jimbo la Tanganyika, Jackson Maneno, Askofu wa Jimbo la Mashariki, Eliasaph Mathayo, Askofu wa Jimbo la Magharibi,  Simon Bikatagu na Askofu wa Jimbo la Kati, Shem Mwenda.