Watanzania wasiokuwa na uwezo wamesaidiwa kupata matibabu Muhimbili

Muktasari:

Balozi wa Saudia Arabia nchini, Mohamed bin Mansour Al-Malik amesema Serikali ya Tanzania na Saudia zinaendelea kuimarisha uhusiano

Dar es Salaam. Balozi wa Saudia Arabia nchini, Mohamed bin Mansour Al-Malik amesema Serikali ya Tanzania na Saudia zinaendelea kuimarisha uhusiano wake kupitia ushiriki wa huduma mbalimbali kwa watanzania wasiokuwa na uwezo wa kulipia gharama ikiwamo za mahitaji ya afya.

Balozi Al-Malik ametoa kauli leo Jumamosi(Novemba 18, 2017) jijini Dar es Salaam wakati wa tukio la kufunga huduma ya bure ya upasuaji wa kuzibua mishipa ya moyo iliyoziba  kwa kutumia mshipa wa damu wa mkono (Catheterization) iliyotolewa na madaktari watatu kutoka Saudia Arabia.

Huduma hiyo inayotolewa kupitia ushirikiano wa  Madaktari bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete(KKCI) ,tayari imehudumia wagonjwa 33 kati 50 wanaotarajia kufikiwa huduma hiyo.

"Ni jambo la kujivunia katika mahusiano yetu na Tanzania, hii inatafsiri uhusiano unaolenga kuokoa maisha ya watanzania na Saudí Arabia haitaishia hapa, huu ni mwanzo tu, tutajielekeza huduma zetu katika sekta nyingine za kijamii ili kuimarisha uhusiano," amesema Balozi Al-Malik.

Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Kimataifa ya Kiislamu ya Misaada(IIRO),Ofisi za Tanzania ambao ni wafadhili  waliowaleta Madaktari hao, Hassan Ahmed Katungunya amesema gharama za matibabu hayo Kwa mgonjwa mmoja ni wastani wa Sh30milioni.

"Kuhusu gharama za kuwaleta Madaktari hao kwa sasa sina taarifa zake lakini, gharama zote zinasimamiwa na IIRO, "amesema.

Katika tukio hiyo, Balozi Al-Malik alikuwa ameongozana na Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar   Zuberi, uwakilishi kutoka Wizara ya Afya pamoja na uongozi wa JKCI.

Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi amesema fedha nyingi zingetumika kulipia gharama za matibabu hayo endapo huduma hiyo isingetolewa kupitia Madaktari hao.

Profesa Janabi amesema upasuaji uliofanyika ni kuwezesha mgonjwa kutoka chumba cha upasuaji akiwa anatembea.

"Na baada ya saa nane kama hali yake itaendelea vizuri anaweza kuruhusiwa, tofauti na upasuaji wa kutumia mshipa wa paja ambao tulikuwa tunafanya, ilikuwa baada ya upasuaji mgonjwa ni lazima akae hospitali kwa zaidi ya saa 24 kuangalia maendeleo yake, "amesema.

Profesa Janabi amesema mbali na huduma hiyo, kambi hiyo ya Madaktari ilihusika na utoaji elimu na kubadilishana  ujuzi wa kazi kati ya wafanyakazi wa taasisi hizo mbili.

"Lakini hata wageni pia wamejifunza vitu vingi na uzoefu mpya wa baadhi ya magonjwa na mambo ya kiteknolojia wasiokuwa nayo kwenye nchi zao, lakini niwaombe wananchi wajenge utamaduni wa Kupima afya zao mara kwa mara,"amesema.

 

Katika tukio hilo, zawadi na tuzo  zilizoandaliwa kwa ajili ya kutambua mchango huo, zimetolewa kwa Wizara ya Afya, JKCI, Madaktari na Uongozi wa IIRO.