Sekta ya uchukuzi yakomba bajeti ya Mawasiliano

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2017/2018, mjini Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Baada ya kuwasilishwa, wabunge waliopata fursa ya kuchangia walieleza kilio cha ubovu wa miundombinu huku wakitaka Ofisi ya Rais (Tamisemi) inyang’anywe barabara na kupewa Tanroads.

Dodoma. Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa ameomba Sh4. 5 trilioni kwa ajili ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2017/18 huku mgawo mkubwa wa Sh2.57 trilioni ukielekezwa kwenye sekta ya uchukuzi.

Baada ya kuwasilishwa, wabunge waliopata fursa ya kuchangia walieleza kilio cha ubovu wa miundombinu huku wakitaka Ofisi ya Rais (Tamisemi) inyang’anywe barabara na kupewa Tanroads.

Katika bajeti hiyo, sekta ya ujenzi inayohusika na barabara imeombewa Sh1.93 trilioni, wakati mawasiliano imeombewa Sh18.1 bilioni.

Pia wizara hiyo imeomba kuidhinishiwa fedha kwa ajili ya shughuli mbalimbali ikiwamo miradi mikubwa ya ujenzi wa barabara, reli na viwanja vya ndege inayoendelea nchini.

Bajeti hiyo ni pungufu kwa Sh400 bilioni ikilinganishwa na iliyopitishwa mwaka jana ya Sh4.9 trilioni.

Katika mgawo huo wa uchukuzi, Profesa Mbarawa alisema, miradi iliyopangwa kutekelezawa ni kuendelea na ujenzi wa reli kwa kiwango cha kisasa (standard gauge) kwa sehemu ya Dar es Salaam hadi Dodoma ambayo imetengewa Sh900bilioni.

Katika mradi huo, mbali na reli ya Dar-Morogoro ambayo imeanza kujengwa, kazi inayoendelea kufanywa na Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (Rahco) ni kuandaa makabrasha ya zabuni kwa ajili ya kuwapata wazabuni.

Ujenzi huo wa reli utaanzia Morogoro hadi Makutopora (Dodoma sawa na kilomita 336), Makutopora hadi Tabora (km 294) na Tabora-Isaka (km 249).

Waziri Mbarawa alisema zabuni zilizotangazwa Novemba, zilifunguliwa Aprili 19, 2017.

Vilevile, Profesa Mbarawa alisema wizara yake inakusudia kujenga au kumalizia ujenzi wa viwanja mbalimbali vya ndege ukiwamo uwanja mpya wa ndege wa Msalato mkoani Dodoma ambao umetengewa Sh5.5 bilioni.

Mbali na uwanja huo, Waziri Mbarawa alisema katika mwaka wa fedha 2017/18, wizara yake itasimamia miradi mbalimbali ya ujenzi wa viwanja vya ndege ukiwamo wa Kigoma, Tabora, Songwe, Mwanza, Arusha, Mtwara, Sumbawanga, Shinyanga na KIA.

Waziri alisema pia kuna mradi wa uendelezaji wa viwanja vya mikoa Geita, Iringa na Ruvuma pamoja na maandalizi ya viwanja vya Ziwa Manyara, Moshi, Tanga, Kilwa Masoko, Lindi, Njombe, Singida na Simiyu.

Meli mpya

Alisema pia zimetengwa Sh3.04 bilioni kwa ajili ya kuanza ujenzi wa meli mpya ya abiria na mizigo katika Ziwa Tanganyika.

Meli nyingine mpya inayojengwa katika Ziwa Victoria imetengewa Sh6.3 bilioni huku ukarabati wa meli ya MV Victoria ukitengewa Sh6 bilioni.

Meli nyingine zilizotengewa fedha kwa ajili ya ukarabati ni Mv Butiama ya Ziwa Victoria (Sh2.5 bilioni), Mv Liemba ya Ziwa Tanganyika (Sh3.77 bilioni), Mv Umoja (Sh1.57 bilioni) na Mv Serengeti zote za Ziwa Victoria.

Kupungua mizigo Bandarini

Pamoja na kutenga fedha za miradi mbalimbali, Waziri huyo amelieleza Bunge jinsi mizigo ilivyopungua kwa asilimia moja bandarini huku akitaja sababu saba za upungufu huo.

Akiwasilisha bajeti hiyo jana, Waziri Mabarawa alisema katika kipindi cha Julai 2016 hadi Februari, Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ilihudumia tani 8.572 milioni ikilinganishwa na tani 8.640milioni zilizohudumiwa katika kipindi hicho mwaka 2015/16.

Hata hivyo, alisema kitengo cha makontena cha Bandari ya Dar es Salaam kilihudumia makontena 106,448 ikilinganishwa na makontena 101,540 yaliyohudumiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2015/16, sawa na ongezeko la asilimia 4.8.

Kwa upande wa kitengo cha makontena (Ticts), alisema makontena yaliyohudumiwa ni 301,555 ikilinganishwa na 317,507 ya mwaka jana sawa na upungufu wa makontena 15,952.

Akizungumzia sababu za upungufu huo, Profesa Mbarawa alisema ni pamoja na kuzorota kwa huduma za Reli ya Tazara kati ya Dar es Salaam na ukanda wa shaba nchini Zambia na utendaji usioridhisha wa Reli ya Kati.

Sababu nyingine ni mdororo wa biashara na shughuli za usafirishaji wa majini, hasa katika ukanda wa Asia unaohudumia meli zinazokuja ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Profesa Mbarawa pia alitaja ushindani kutoka bandari nyingine unaotokana na kuimarika kwa miundombinu ya reli na bandari za Beira na Nacala nchini Msumbiji, hivyo kuvutia baadhi ya wateja wa Zambia na Malawi.

Sababu nyingine ilitajwa kuwa ni usumbufu na udanganyifu kwa wateja kutoka kwa wakala wa forodha na uondoshaji shehena.

Jambo jingine lililopunguza mizigo ni kuanzishwa kwa himaya moja ya forodha kwa nchi zisizo wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakati bandari shindani kama za Mombasa, Beira, Nacala, na Durban hazitumii mfumo huo.

“Hii imepunguza sana kiasi cha shehena inayohudumiwa kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Jambo jingine alisema ni sheria za hapa nchini kutoruhusu matumizi ya magari makubwa katika barabara zake tofauti na nchi nyingine shindani.

Wabunge waja juu

Wakichangia bajeti hiyo, wabunge wameitaka Tamisemi, inyang’anywe barabara na kupewa Tanroads.

Wabunge karibu wote waliopata nafasi ya kuchangia katika hotuba ya bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano walijikita katika kuhoji ni lini barabara za maeneo yao zitakamilika.

Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CCM) Peter Serukamba alisema katika bajeti hiyo amesikia kuwa Serikali inakusudia kuanzisha wakala wa barabara vijijini.

Alisema kuwa kuanzisha wakala huyo ni kuongeza matumizi ya Serikali na kushauri barabara zote kuhamishiwa Tanroads.

“Sasa hivi Tanroads wanapatiwa asilimia 60 ya fedha za Mfuko wa Barabara badala ya kuanzisha wakala wa barabara vijijini ni vyema fedha zote zikaenda Tanroads na Tamisemi wanyang’anywe barabara zote kwanza wana mambo mengi,” alisema.

Mbunge wa Kavuu (CCM), Dk Pudensiana Kikwembe alihoji kuhusu ujenzi wa Barabara ya Mpanda-Tabora hadi Sikonge umefikia wapi wakati tayari watu mbalimbali walikubali kusaidia ujenzi wake.

“Kigugumizi kiko wapi? Wakati Rais John Magufuli akiwa waziri alinishirikisha katika mazungumzo na ADB (Benki ya Maendeleo Afrika) ilishakubali,” alihoji.

Mbunge wa Mafia (CCM), Mbaraka Kitwana aliitaka Serikali iharakishe ujenzi wa barabara isije kukumbwa na tatizo la ukosefu wa udongo katika eneo hilo.