Monday, June 19, 2017

Sendeka atumia msiba wa mama yake kutuma salamu kwa Lowassa

 

By Joseph Lyimo, Mwananchi jlyimo@mwananchi.co.tz

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka amemtuma Mbunge wa Simanjiro, mkoani Manyara (Chadema), James Ole Millya kumpelekea salamu za shukrani, Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa kwa kitendo chake cha kumuunga mkono Rais John Magufuli, katika jitihada zake za kulinda rasilimali za Taifa.

Akizungumza jana kwenye mazishi ya mama yake mzazi, Raheli Sendeka yaliyofanyika kwenye Kijiji cha Losokonoi wilayani Simanjiro, Ole Sendeka alisema ni jambo zuri kwa Lowassa kuunga mkono jitihada za dhati za Rais Magufuli kulinda rasilimali za nchi.

Alisema baada ya kusoma magazeti kuwa Lowassa amempongeza Rais Magufuli naye hana budi kumpongeza Lowassa kwa hilo.

“Nanyi wabunge mkiwa bungeni muungeni mkono Rais wetu Magufuli anavyotetea rasilimali za nchi ili madini yanayochimbwa yaweze kuwanufaisha Watanzania, waweze kupata huduma zao za msingi kupitia madini yao,” alisema Ole Sendeka.

Pia, aliwashukuru wabunge waliohudhuria mazishi hayo, akiwamo Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu, Profesa Norman Sigala, Mbunge wa Babati Vijijini, Vrajlal Jituson na Ole Millya na kuwataka waendeleze umoja kwa kutetea masilahi ya jamii wakiwa bungeni.

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Kati, Dk Solomon Masangwa alisema Watanzania wanapaswa kuuenzi upendo walioachiwa na Mungu.

Alisema japokuwa kuna msemo usemwao amani haipatikani ila kwa ncha ya upanga, Watanzania wasikubali hilo kwa kudumisha umoja uliopo ili kuendeleza amani iliyopo.

Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William Ole Nasha akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Serikali alisema jamii inapaswa kumuenzi marehemu Raheli Sendeka kwa kuiga yale yote mema aliyokuwa anayafanya kipindi cha uhai wake.

Ole Millya alisema wakati aliposhinda ubunge wa Simanjiro aliahidi kuwapenda na kuwapa ushirikiano wananchi wote wa wilaya hiyo bila ubaguzi wowote.

“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe, niliahidi kutobagua watu kwenye uongozi wangu na hivi ndivyo ninavyofanya ili kuweka pamoja jamii yetu ya Jimbo la Simanjiro,” alisema Ole Millya.

Akisoma historia ya mama yake, Sumleck Ole Sendeka alisema Raheli alizaliwa mwaka 1927 huko Oleng’iding’idata, Kijiji cha Lendanai wilayani Simanjiro.

Alisema Raheli aliolewa na baba yao akiwa mke wa kwanza kati ya wanane wa marehemu baba yao Mzee Olonyokie Ole Sendeka na alijaliwa watoto 12, kati yao saba wako hai na watano walishafariki dunia. Alisema marehemu ameacha wajukuu 137, vitukuu 93 na kilembwe mmoja.

Alisema marehemu alibatizwa mwaka 1971 KKKT, Mtaa wa Orkesumet Usharika wa Naberera.

Alisema marehemu alianza kusumbuliwa na kisukari mwaka 2000 na kupata matibabu hospitali za KCMC, Mount Meru, Siima, St Thomas, Calvary Mirerani, Losokonoi na Lendanai hadi alipoaga dunia saa sita usiku, Juni 9.

-->