Breaking News
Thursday, January 11, 2018

Serengeti maarufu kwa kunyonya, kuhifadhi hewa ya ukaa

 

By Anthony Mayunga, Mwananchi

Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ni maarufu duniani kwa kunyonya na kuhifadhi hewa ya ukaa ambayo inazalishwa katika mataifa mbalimbali na ni hatari kwa maisha ya wanyama na binadamu.

Hewa ya Ukaa ina madhara makubwa duniani kwa kuwa inatoboa tabaka la Ozori, miale mikali ya jua inafikia uso wa dunia na kusababisha ongezeko la joto na maradhi ya Kansa,na huzalishwa sana wakati wa uzalishaji wa nishati toka vyanzo vya makaa na mafuta.

Hifadhi hiyo ambayo ni miongoni mwa maajabu saba ya dunia kutokana na wanyama kama nyumbu na Pundamilia wanaohama kwa makundi makubwa kwenda na kurudi hifadhi ya Maasai Mara Nchini Kenya kwa kuvuka Mto Mara.

Mkuu wa Kitengo cha Utafiti wa Wanyamapori Tanzania(Tawiri)Kituo cha Serengeti Robert Fyumagwa anasema,hifadhi hiyo ni muhimu sana kwa kunyonya kiasi kikubwa cha hewa ya ukaa kinachozalishwa katika mataifa mbalimbali duniani.

“Wastani wa tani 420 hunyonywa katika hekta ambayo ina wanyamapori wakazi wasiopungua 20 wanaokula majani,hifadhi ya Taifa ya Serengeti ina wanyama wengi ndiyo maana ina uwezo mkubwa wa kupunguza hewa ya Ukaa kidunia,”anasema.

Anasema Hewa hiyo inazalishwa na mataifa mengi duniani yaliyoendelea ambayo yana viwanda vingi,hewa hiyo ina madhara makubwa kwa viumbe wote wakiwemo wanyama pia kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.

“Kila mtu ana wajibika kupambana na watu wanaoua wanyamapori,licha ya kuingiza fedha nyingi za kigeni lakini wanasaidia kupunguza madhara makubwa kwa watu yanayotokana na uzalishwaji wa hewa ya Ukaa,”anabainisha.

Anasema wingi wa wanyama na mazingira yaliyohifadhiwa vema ni chanzo kizuri cha kupunguza hewa hiyo ambayo inasambaa kwa kasi kutokana na kazi nyingi zinazofanyika hasa za viwanda na magari kwa mataifa yaliyoendelea.

Muikolojia wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti Emiliana Kihwele anasema duniani hakuna hifadhi yenye uwanda wenye nyasi nzuri kama Hifadhi ya Taifa ya Serengeti,hali hiyo inaifanya kidunia iwe maarufu kwa unyonyaji wa hewa ya ukaa.

“Nyasi na miti mchana huvuta hewa ya ukaa kwa ajili ya kutengeneza chakula,hifadhi hiyo yenye utajiri wa vitu vyote inasaidia kwa sehemu kubwa kupunguza madhara kwa binadamu ambayo yanachangiwa na maendeleo ya mataifa yaliyoendelea kiviwanda,”anasema.

Hata hivyo anakiri kuwa uchomaji moto maeneo yaliyohifadhiwa kuna athari kubwa kimazingira,”wataalam wanasema moto ndani ya hifadhi za Taifa si mzuri kwa kuwa unaathiri mfumo wa uvutaji wa hewa ukaa,hata hivyo kiilojia moto unatakiwa sana ili iendelee kuwepo,”anasema mtaalam .

Athari yake.

Hewa ya Ukaa inasababisha ongezeko la joto duniani,Mabadiliko ya Tabia nchi na Ukame,mvua zisizotabirika,mafuriko na majanga mbalimbali kama mafuriko.

“Hewa ya Ukaa ni moja ya gesi zilizoko angani ambazo zinapasha joto Ozone Layer(blanketi)ambalo hutoboka na matokeo yake mionzi mingi hufika duniani na kurudi angani na husababisha madhara kwa viumbe waishio duniani,”anabainisha.

Anasema hewa hiyo inasababisha ongezeko la joto duniani,mabadiliko ya tabia nchi,ukame ,mvua zisizotabirika na majanga mbalimbali kama mafuriko na athari zake ni kubwa kiafya.

Kwa mjibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO)linasema ongezeko la joto duniani linaweza kusababisha ongezeko kubwa la magonjwa wanaosababishwa na wadudu.

Madhara kwa watoto yanatarajiwa moja kwa moja kutokana na hali ya angani na husababisha majeraha na vifo,ongezeko la maradhi yanayotokana na uchafuzi wa hewa,na huchangia ongezeko la udhaifu dhidi ya watoto ukilinganisha na makundi mengine.

“Ongezeko la joto Duniani linachangia kupunguza upatikanaji wa maji safi na chakula barani Afrika na Asia,majanga,vurugu na magonjwa yanazidi kuongezeka kuwa mengi na makali zaidi,”anabainisha

Kwa upande wake Kihwele anasema uharibifu wa mazingira wa maeneo yaliyohifadhiwa umeathiri vijiji vingi vilivyoko kando ya maeneo hayo kwa kukosa vyanzo vya maji na hata upande wa mavuno si mzuri.

Wazalishaji wakubwa.

Marekani na China ni wazalishaji wakubwa wa Hewa ya Ukaa na zinaungana na mataifa Mengine kama India ,Pakstani,Iran,Iraq na nchi za Ghuba ambazo zimeweka mkakati wa kuacha uzalishaji mwaka 2028.

Hata hivyo China ambayo ni mzalishaji mkubwa imeahidi kuanzia mwaka 2029 itapunguza uzalishaji,makubaliano yakitekelezwa inakadiriwa karibu tani bilioni 70 za hewa ya ukaa zitaondolewa katika uso wa dunia ifikapo mwaka 2050.

Mifugo ni hatari.

Fumagwa anasema maeneo ambayo yana mifugo mingi uzalishaji wa hewa ya ukaa ni mkubwa,”mifugo inaua uoto wa asili na inaacha ardhi wazi ,na vinyesi vilivyorundikana vinazalisha Methane inayoongeza hewa ya ukaa,”anasema.

Mikakati.

Mtafiti huyo anasema kuwa Jumuiya ya Kimataifa imeanisha mbinu za kupunguza hewa ya Ukaa ikiwa ni pamoja na kutumia nishati jadidifu,kama matumizi ya viwanda vya kisasa vinavyozalisha hewa ya ukaa kidogo,kupanda miti,kutokuchoma mioto au kutokata miti ovyo.

Hata hivyo anasema kuwa mataifa tajiri kama Marekani hawajaridhia mkakati huo wa pamoja wa kupunguza hewa ya ukaa,hali ambayo inatishia afya za watu na wanyama.

Marekani na China zinatoa gesi joto kwa wingi kutokana na wingi wa viwanda,pamoja na kuwepo kwa mapendekezo ya nchi matajiri kupunguza zaidi matumizi ya gesi ya Hydrofluro carbon(HPCs) na zaidi ya nchi 150 zimefikia makubaliano hayo kuanzia mwaka 2019 kwa asilimia 10.

“Uhifadhi una faida kubwa mbali na kipato lakini tunapata faida ya kupunguza hewa ya ukaa,kwa hifadhi zote,mapori ya akiba,mistu ya asili na ya kupandwa,na Tanzania tuna utajiri mkubwa wa maeneo yaliyohifadhiwa na tunapaswa kuyalinda,”anabainisha.

Hata hivyo baadhi ya wataalam wa mazingira wanasema kuwa viwango vya hewa ya Ukaa anga la juu ni vya juu kuliko miaka 800,000 iliyopita,ni wajibu wa kila mmoja ni kuongeza matamanio kwa mambo makuu matano,ya Utoaji wa hewa chafuzi,kukabili madhara ,fedha , ubia na uongozi.

Anasema ongezeko la mauaji ya wanyama na uharibifu wa mazingira ni hatari kubwa kwa nchi kwa kuwa uwezo wa kuhifadhi hewa ya Ukaa unapungua na athari zake zinahamia kwa binadamu na wanyama kiafya.

Umuhimu mwingine.

Kwa mjibu wa mtafiti huyo hifadhi hiyo ni muhimu sana kwa kutunza vimelea hatari vya magonjwa kama Kimeta,ugonjwa wa midomo na miguu na mengine yasiweze kudhuru binadamu na wanyama.

“Kuna vimelea vinavyotokana na wanyama ikiwemo kichaa kinachosambazwa na wanyama kama Fisi na vicheche ni hatari sana kwa maisha ya binadamu,katika hifadhi hii utafiti umebaini kuwa vimelea hivyo vinatuzwa na havisambai,huu ni umuhimu wa kipekee na unazidisha umaarufu wa hifadhi ya Taifa ya Serengeti,”anasema.

Na hiyo inatokana na mazingira wanayoishi wanyama hao,mfano nyati wanakupe nyingi lakini hawana madhara,lakini wanyama wafugwao wakishambuliwa na kupe hao hupata madhara makubwa ikiwemo vifo.

Ikolojia ya Serengeti yenye eneo la zaidi ya kilometa 30 inajumuisha Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ,Mapori ya akiba ya Ikorongo na Grumeti,Maswa na Kijereshi,Pori tengefu la Loliondo,Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro,Hifadhi za Jamii za Ikona,Makao na Masai Mara nchini Kenya. 

-->