Serikali: Malipo ya mawakala ni baada ya uhakiki

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji akijibu hoja za wabunge waliochangia mjadala wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka wa fedha 2018/2019, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Kauli hiyo imetolewa leo bungeni baada ya wabunge kulalamikia mawakala hao kucheleweshewa malipo


Dodoma. Serikali imesema itawalipa mawakala wote wa pembejeo za kilimo baada ya vyombo vya uchunguzi kukamilisha uchunguzi wa watumishi waliodanyanga kuhusu malipo na uhakiki wa madeni unaendelea.

Akijibu baadhi ya hoja za wabunge waliozitoa wakati wakijadili bajeti ya wizara ya kilimo ya mwaka 2018/19, leo jioni Mei 16, 2018, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji amesema malipo ni mara baada ya uchunguzi kukamika.

“Nani kaiibia Serikali, katika maombi haya vyombo vya uchunguzi vipo kazini, sisi kama wabunge wasimamizi wa rasilimali, vyombo vya uchunguzi ni muhimu na kama ni mtumishi nani aliongeza sifuri katika milioni 20 ikawa bilioni, fedha si tatizo na tutawalipa wote wanaoidai Serikali,” amesema Dk Kijaji

Kuhusu kutengwa kwa bajeti kidogo, Dk Kijaji amesema Serikali inatambua umuhimu wa sekta ya kilimo lakini utengaji wa bajeti unategemea rasilimali zilizopo.

“Rasilimali ziko chache kuliko mahitaji, sote tupo hapa, mlisema bajeti ya afya iongezwe, maji iongezwe na ifahamike Serikali inatoa kipaumbele kwa kilimo na sisi tunatambua kuwekeza katika kilimo,” amesema Dk Kijaji

Amesema miongoni mwa jitihada hizo ni kuiwezesha Benki ya Kilimo: “Tumewekeza Sh60 bilioni na mpaka sasa wana Sh66 bilioni, wameweza kuongeza kiwango hiki katika utendaji wetu na tumechukua mkopo zaidi ya Sh250 bilioni na kuipa benki hii.”

Akigusia benki hiyo kuwa jijini Dar es Salaam, amesema mwezi huu itafungua tawi jijini Dodoma, Juni jijini Mbeya na Julai jijini Mwanza na dhamira yetu ni kuwafikia wananchi kule waliko.

Kwa upande wake, Naibu waziri wa Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Joseph Kakunda ametoa maagizo kwa maofisa kilimo kutoka ofisini na kwenda kuelimisha wakulima na wale watakaoshindwa watachukuliwa hatua.

“Lazima wakulima wapate haki yao ya elimu kuhusu kilimo na utaratibu wa kusubiri posho ili aende kufanya kazi yake tumeshapiga marufuku,” amesema Kakunda.

Kakunda amesema, “maofisa ushirika lazima wahakikishe wanafanya mapitio ya vyama vya ushirika ili kujua kama utendaji ni mzuri na kama ni mbovu wavifute na kuvisajili upya.”

“Maofisa ugani wafanye kazi ya kuwatambua wakulima wote ili Serikali ifanye maandalizi ya haraka ya kuandaa pembejeo, walio chini ya Tamisemi wapate huko hizi taarifa na uzembe hautavumiliwa,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso amesema Serikali imetenga zaidi ya Sh29 bilioni kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na, “sisi kama wizara tutalisimamia hili na tunaahidi kushirikiana vizuri na wadau wa wizara ya kilimo.”