Serikali, wafanyabiashara wafungua ukurasa mpya

Muktasari:

Wiki iliyopita Rais Magufuli alimuagiza Dk Mpango kufuatilia kodi inayotozwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) huku akikerwa na baadhi ya watumishi wa mamlaka hiyo wasiowaaminifu wanaowabambikia wafanyabiashara kodi.

 Siku nne baada ya Rais John Magufuli kumwagiza Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk Philip Mpango kufuatilia kero katika utozaji wa kodi, wafanyabiashara wamemweleza mkuu huyo wa nchi kwamba changamoto hiyo imesababisha wengi wafunge biashara zao.

Wiki iliyopita Rais Magufuli alimuagiza Dk Mpango kufuatilia kodi inayotozwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) huku akikerwa na baadhi ya watumishi wa mamlaka hiyo wasiowaaminifu wanaowabambikia wafanyabiashara kodi.

Akiweka jiwe la msingi katika ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Morogoro hadi Makutupora mkoani Dodoma, Rais Magufuli alisema baadhi ya watumishi wa TRA wamekuwa wakiipaka matope Serikali kwa kuwabambikia kodi wafanyabiashara huku wakiitumia vibaya kauli ya ‘Hapa Kazi Tu’

Jana, katika mkutano wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) uliofanyika chini ya uenyekiti wake, wafanyabiashara walilalamikia kodi kama miongoni mwa kero kuu katika kufanya biashara.

Mmoja wa wafanyabiashara ambaye anamiliki kiwanda cha Mvinyo mkoani Dodoma aliyejitambulisha kwa jina moja la Minde alisema chupa zake zimekwama bandarini kwa sababu anadaiwa kodi kubwa.

Alisema kontena lenye chupa za mvinyo lililoingizwa nchini limekwama bandarini kwa sababu wamekuwa wakitofautiana na TRA.

Alisema alinunua chupa hizo kwa Euro 16,000 (Sh45 milioni) lakini mamlaka hiyo inasema chupa hizo ni za Euro 25,000 (Sh69.5 milioni).

“Nimewaonyesha nyaraka zote za ununuzi wa mzigo huo, lakini wapi hawataki kunielewa wamezuia mzigo wangu,” alisema mama huyo.

Alisema lengo la mamlaka hiyo ni kumtaka alipie kodi kubwa kuliko inavyotakiwa.

Alisema biashara zake zinakwama kwa sababu ya kukosekana kwa chupa hizo kiwandani kwake.

Baada ya kuyasema hayo, Rais Magufuli aliagiza mamlaka hiyo kuruhusu kontena lenye chupa za mvinyo za kiwanda cha Dodoma lililokwama bandari zitolewe leo.

Magufuli aliiagiza TRA kutoza kodi inayolingana na Euro 16,000 alizonunulia mzigo huo badala ya Euro 25,000.

Mfanyabiashara mwingine kutoka Arusha, Aloyce Mangapi alisema mamlaka hiyo imekuwa ikikadiria kodi ambazo hazilingani na uhalisia.

“Wafanyabiashara Kariakoo (Dar es Salaam), Arusha na Mwanza wamefunga maduka yao kwa sababu ya kodi zinazoumiza, ni kama TRA wanawakomoa wafanyabiashara,” alisema.

Alimshukuru Rais Magufuli kwa kulishtukia jambo hilo hata hivyo alisema amechelewa kwa sababu wafanyabiashara wengi wameshafunga maduka kwa kero hiyo.

“Baadhi wamefunga maduka kwa sababu ya kodi, ajira za watu zimepotea, hali ni mbaya,” alisema.

Aliomba kuwe na mfumo rafiki kwa mamlaka hiyo kuwatoza kodi wafanyabiashara ili waifurahie hali hiyo badala ya kuwa karaha.

Mfanyabiashara wa Kilimanjaro, Patrick Msuya alisema kumekuwa na utitiri wa tozo za kodi ambazo nyingine hazitozwi na TRA

“Mheshimiwa Rais kuna utitiri wa tozo ambazo nyingine hazitozwi na TRA zinatozwa na mamlaka nyingine za Serikali,” alisema.

Aliongeza: “kodi hizi zinatuchanganya wafanyabiashara, baadhi wanashindwa hata kuzifahamu taasisi hizi zinazotoza.”

Aliiomba Serikali kuweka mfumo mmoja utakaosimamia tozo za kodi ili kuwarahisishia wafanyabiashara kushughulikia masuala ya kikodi.

Majibu ya Magufuli kuhusu kodi

Akizungumza kabla ya kufunga mkutano huo, Rais Magufuli alisema wafanyabiashara wasidhani kwamba Serikali inawachukia kwa sababu ya kero hizo.

“Wafanyabiashara ni wadau wakuu wa Serikali, Serikali inawapenda, tutaendelea kushirikiana,” alisema Magufuli na kuongeza kuwa Tanzania ni nchi nzuri inayofaa kwa uwekezaji.

Alisema kero zote zilizotolewa na wafanyabiashara zikiwemo za kikodi zitapatiwa ufumbuzi katika kipindi kifupi kijacho.

Rais Magufuli alimwelekeza Waziri Mpango kukaa na Kamishna wa TRA, Charles Kichere ili kushughulikia kasoro ambazo zinajitokeza.

“Waziri wa Fedha, Dk Mpango wewe una mamlaka ya kuweza kukaa na wafanyabiashara na kujadili kuhusu kodi wanayodaiwa, wewe una uwezo hata wa kuwapunguzia,” alisema.

Hata hivyo, pamoja na ahadi yake ya kushughulikia kero hizo, Rais aliwataka wafanyabiashara hao kutokwepa kodi ili iweze kuendesha Serikali.

TRA yafungua maduka Lindi

Katika kutekeleza kile Rais alichokizungumza wiki iliyopita, TRA ilitoa tamko la kuyafungulia maduka yaliyofungwa kwa sababu mbalimbali na mamlaka hiyo mkoani Lindi.

Juzi, kamishna wa kodi za ndani TRA, Elijah Mwandubya aliwasimamisha kazi, meneja wa TRA Mkoa wa Lindi, John Msangi na ofisa mkuu wa kodi mkoani humo Alfred Chembo.

Mkurugenzi wa Elimu na Huduma za Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo alisema maduka hayo yamefunguliwa kuanzia Machi 17.

Alipoulizwa sababu za maduka hayo kufungwa na TRA alisema:

“Wewe unapaswa kutambua kuwa maduka hayo tumeyafungua yaendelee kufanya shughuli zake. Hayo ambao yalifungiwa kwa sababu gani si sahihi kwa sasa. Kama kuna waliofunga wenyewe kwa sababu zao, hatuwezi kuwataka wafungue na kuendelea na shughuli zao.”

Hatua ya TRA ilipongezwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye katika mkutano huo alisema Serikali itahakikisha inasimamia haki za wafanyabiashara wote nchini.

“Hatuwezi kukubali watumishi wachache waipake Serikali yetu matope kwa kufanya vitendo vinavyokiuka sheria na taratibu,” alisema.

Kamishana Mkuu wa TRA, Charles Kichere alipozungumza na Mwananchi hivi karibuni baada ya Rais kuishukia mamlaka hiyo alisema ameyapokea kwa unyenyekevu mkubwa na ameahidi kuyafanyia kazi kwa kuongeza elimu kwa walipa kodi ili wajue haki na wajibu wao.

“Wakati mwingine mtu anapata kero kwa kuwa hana elimu ya mlipakodi hivyo haujui wajibu na haki yake, Kwa kulitambua hilo tulianzisha wiki ya elimu kwa mlipa kodi kila mwaka na leo Mheshimiwa Rais ametupatia maagizo mengine nayo tunayafanyia kazi.”

Alisema changamoto za kodi zimekuwepo kila siku na kuna baadhi ya walipakodi hufika ofisini kwake na malalamiko mbalimbali, “Wakija ofisini tunaongea nao tunaangalia namna ya kutatua changamoto husika tunasonga mbele”.