Serikali ‘yaiua’ rasmi TTCL

Dodoma. Serikali imewasilisha muswada wa sheria ambao unaiua rasmi Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) na kuanzisha shirika jipya la mawasiliano ambalo litamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100.

Muswada huo uliwasilishwa jana bungeni na waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa huku wabunge wakipinga baadhi ya vifungu.

Akiwasilisha muswada huo, Profesa Mbarawa alisema madhumuni yake ni kuanzisha shirika hilo kwa ajili ya kulinda usalama wa nchi, kukuza uchumi na kutoa huduma kwa jamii.

Profesa Mbarawa alisema sheria hiyo mpya italiwezesha shirika hilo kutekeleza majukumu yake kama shirika la umma la mawasiliano likijulikana kama Tanzania Telecommunication Corporation.

Alisema mambo muhimu ya kuzingatiwa katika muswada huo ni kuwa unakwenda kuifuta TTCL na kuanzisha shirika jipya.

Muswada huo wa sheria ambayo itatumika Tanzania Bara na Zanzibar umependekeza muundo, mtendaji mkuu na wajumbe watano ambapo upande wa Zanzibar utakuwa na mjumbe mmoja. Kwa mujibu wa muswada huo, ili mtu awe na sifa ya kuteuliwa kuwa mtendaji mkuu ni lazima awe na uzoefu wa miaka minane katika ngazi ya juu ya utawala.

Hata hivyo, wabunge waliungana kutaka Zanzibar iwe na wajumbe wawili badala ya mmoja katika bodi ya wakurugenzi na wakataka pia uzoefu wa mtendaji mkuu uwe miaka mitano badala ya minane.

Mbali na suala la uwakilishi wa Zanzibar, wabunge wa CCM na wale wa upinzani waliungana pia kutaka waziri asiwe na madaraka makubwa ya kuingilia uendeshaji wa shirika hilo. Vilevile wabunge karibu wote waliochangia pamoja na kambi rasmi ya upinzani bungeni, wakasisitiza juu ya Zanzibar kupewa nafasi mbili kati ya tano badala ya moja ili kuleta sura halisi ya Muungano.

Hata hivyo, Naibu Spika Dk Tulia Ackson alitahadharisha mwelekeo wa mjadala huo akisema hilo si shirika la kwanza la Muungano, hivyo wasije wakaanzisha utaratibu mpya kwenye mashirika.

Akiwasilisha hotuba ya msemaji wa Kambi ya Upinzani Bungeni, mbunge wa viti maalumu (Chadema), Dk Immaculate Sware alitaka bodi ya wakurugenzi ya shirika iwe na sura ya Muungano.

Kambi hiyo pia ilipinga kifungu cha 7(7) cha muswada huo kinachompa waziri madaraka, ikisema mamlaka hayo makubwa yanaweza kutumika ikiwa hakutakuwa na jicho la pili.

Hoja hiyo iliungwa mkono pia na Kamati ya Bunge ya Miundombinu katika taarifa yake iliyowasilishwa na mwenyekiti wake, Profesa Norman Sigala. “Ili shirika liweze kufanya kazi vizuri, ni vyema bodi na mtendaji mkuu wa shirika wapewe madaraka kamili ili watumie uwezo wao kuleta maendeleo ya shirika,” alisisitiza Profesa Sigala.

Akichangia muswada huo, mbunge wa Welezo (CCM), Saada Mkuya alisema shirika hilo jipya ni la Muungano, hivyo akapendekeza kuwepo mkurugenzi mkazi Zanzibar ambaye atakuwa Mzanzibar.