Serikali haina mpango na maziwa ya mende

Muktasari:

Kauli hiyo ya Serikali imekuja baada ya timu ya kimataifa ya wanasayansi kubaini chembechembe za protini ndani ya mende aina ya diploptera punctuate ambaye huzaa watoto tofauti na aina nyingine.

Dar es Salaam. Siku chache baada ya utafiti kubaini wingi wa protini katika maziwa yanayoweza kutolewa kutoka aina mpya ya mende, Serikali imesema haina mpango na maziwa hayo kwa sasa.

Kauli hiyo ya Serikali imekuja baada ya timu ya kimataifa ya wanasayansi kubaini chembechembe za protini ndani ya mende aina ya diploptera punctuate ambaye huzaa watoto tofauti na aina nyingine.

Mratibu wa kitaifa wa uongezaji wa virutubisho katika chakula kutoka Taasisi ya Chakula na Liche (TFNC), Celestine Mgoba alisema licha ya kutofahamu utafiti huo, bado mende hakubaliki kwa jamii ya Watanzania kama chakula.

“Wala hatuna mpango na matumizi ya mende kwenye vyakula. Ni mpaka utafiti ufanyike na Serikali itoe kibali. Inawezekana mtu tu amefanya utafiti wake, ni mpaka uthibitishwe.” alisema Mgoba.

 “Kitu chenyewe mende? ukiwaambia watu kuhusu ubora wa maziwa ya mbuzi tu inakuwa shida? Wengi wanataka ya ng’ombe, ndiyo utakuja kusema mende? Halafu hao mende watatoa maziwa mengi kiasi gani, maana yanatakiwa mengi.”