Serikali kuandaa maonyesho ya kuwatambua wabunifu

Muktasari:

Wabunifu wametakiwa kujitokeza na kuonyesha vipaji vyao

Dodoma. Serikali inakusudia kuandaa maonyesho ya wabunifu mbalimbali nchini lengo likiwa ni kuwatambua na kushiriki katika uchumi wa viwanda.


Akizungumza leo Ijumaa Juni 23, 2018 mjini hapa wakati akifunga mafunzo mradi wa Kukuza Ujuzi na Stadi za Kazi (ESPJ), Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa James Mdoe amewataka wabunifu mbalimbali nchini kujitokeza na kuonyesha vipaji vyao badala ya kuvificha.


“Katika mwaka wa fedha 2018/19 Serikali itaandaa maonyesho makubwa kwa ajili kutoa fursa kwa wabunifu mbalimbali kuonyesha vipaji vyao ili waweze kutambulika,” amesema.


Amesema mradi wa ESPJ unaotekelezwa na Serikali kupitia wizara hiyo na Benki ya Dunia (WB), ulianzishwa kwa kutambua kuwepo kwa wabunifu mbalimbali nchini licha ya kuwa wengine hawajulikani na hivyo vipaji vyao kufichika.


“Kwa kuliona hilo ndio mana serikali imeamua kuandaa onyesho hilo ili iweze kuwatambua wabunifu hao na ubunifu wanaoufanya kwa lengo la kuchangia katika uchumi wa Taifa,”amesema.


kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo,  Avemaria Semakafu amesema wapo watoto ambao wameanza ubunifu tangu shule ya msingi, hivyo ni vyema vipaji hivyo vikakuzwa.

Mratibu wa mradi wa ESPJ, Osward Lukonge, amesema mradi huo umegharimu kiasi cha dola za Marekani milioni 250.


amesema kati ya hizo, Serikali imetoa dola za Marekani Milioni 130 na WB imetoa dola za Marekani milioni 120.


Amebainisha kuwa lengo la mradi huo ni kuwawezesha vijana kupata ujuzi kwa vitendo na sio kwa nadharia.


“Matarajio ni kuwa na ongezeko la vijana wenye ujuzi unaotakiwa kulingana na soko la ajira,”amesema.


Hata hivyo, Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya mradi huo, Ngwisa Mpembe, amesema katika utekelezaji wa mradi huo wanakabiliwa na changamoto ya rasilimali fedha.


Mpembe amesema kwa sasa Serikali inachangia kwa asilimia 70 ambayo haitoshelezi.