Serikali kuchunguza sakata la Watanzania Msumbiji

Katibu Mkuu wa wizara ya mambo ya ndani ya nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira

Muktasari:

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Meja Jenerali Projest Rwegasira alisema wizara inaendelea na uchunguzi ili kujiridhisha na madai hayo kabla taratibu za kidiplomasia hazijachukuliwa baina ya nchi hizo mbili.

Dar es Salaam. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, imesema inaendelea na uchunguzi kuhusu madai ya kufanyiwa ukatili kwa Watanzania waishio nchini Msumbiji huku ikidai kurejeshwa kwao ni halali endapo walivunja taratibu za uhamiaji.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Meja Jenerali Projest Rwegasira alisema wizara inaendelea na uchunguzi ili kujiridhisha na madai hayo kabla taratibu za kidiplomasia hazijachukuliwa baina ya nchi hizo mbili.

Awali, zilieleza kurejeshwa kwa Watanzania takribani 180 huku kukiwa na madai ya kufanyiwa vitendo vya kikatili ikiwamo kuchaniwa hati za kusafiria, kuporwa mali na kuacha biashara zao.

Kuhusu suala hilo, Rwegasira alisema malalamiko yapo, lakini kwa upande mwingine yanaweza kuwa ni ya kweli au siyo kwa kiwango kinachodaiwa hivyo uchunguzi zaidi utafanyika.

“Uchunguzi zaidi utafanyika ili kubaini vitendo hivyo. Siwezi kujua sheria za Msumbiji zinasemaje lakini baada ya uchunguzi hatua za kidiplomasia zitafuatwa,” alisema.

“Ni haki ya kila nchi kuona wageni wanafuata sheria na kanuni za uhamiaji. Kurudishwa kwa Watanzania siyo jambo geni hata sisi tunafanya ili kuwabaini pale inapobidi,” alisema.

Alisema kuwa mwaka 2013, nchi ilifanya operesheni Kimbunga huko mkoani Kagera ambapo watu 37,000 waliokuwa wakiishi kinyume na sheria walirudishwa huku kukiripotiwa malalamiko kama hayo.

Meja Jenerali Rwegasira alitoa wito kwa Watanzania wote wanaotaka kwenda nchi za nje kufanya kazi, biashara au shughuli yoyote halali wafuate sheria ili kuepukana na adha kama hizo.

Operesheni hiyo inaendeshwa katika mji wa Monte Puez uliopo Jimbo la Cabo Delgado ambapo zaidi ya Watanzania 3,000 wanaishi huko hali inayoashiria kuwa idadi inaweza kuongezeka.