Serikali kulipa Sh43.39 bilioni za madai ya watumishi

DK MPANGO ATANGAZA NEEMA KWA WALIMU NA WATUMISHI WA UMMA

Muktasari:

Wenye madai zaidi ya miaka 10 nao wapo katika orodha hiyo.


Dodoma. Serikali imesema malimbikizo ya madai ya watumishi wa umma yenye thamani ya Sh 43.39 bilioni yatalipwa pamoja na mshahara wa Februari, 2018 kwa mkupuo mmoja.

Akizungumza leo Februari 9, 2018 na waandishi wa habari bungeni mjini Dodoma, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema fedha hizo zinajumuisha madai ya watumishi ya zaidi ya miaka 10 iliyopita, kwamba majina ya watakaolipwa yatatangazwa kwenye magazeti kuanzia kesho Februari 10, 2018.

Amesema Serikali kupitia mfumo wa taarifa za kiutumishi na mishahara hadi kufikia Julai Mosi mwaka jana ilikuwa na madai ya mishahara yenye jumla ya Sh 127.6 bilioni kwa watumishi 82,111.

Amesema kati yao ni walimu 53,925 waliokuwa wakidai Sh 53.9 bilioni ambayo ni sawa na asilimia 42.27 ya madai yote na wasiokuwa walimu 28,186 waliokuwa wakidai jumla ya Sh73.6 bilioni sawa na asilimia 57.7

ya madai yote.

“Madai haya yalikuwa ya muda mrefu mengine yakiwa ya kuanzia mwaka 2005 hadi mwaka 2017,” amesema.

Amesema madai hayo yalijumuisha mishahara isiyolipwa, tofauti ya mishahara isiyolipwa, tofauti ya mishahara kutokana na kukaimu na

nyongeza za mishahara zilizotokana na kupandishwa na kuchelewa kurekebishiwa mishahara.

Dk Mpango alisema madai ya watumishi 27,389 kati ya 82111 yenye jumla ya Sh 43.39 bilioni ikiwa ni sawa na asilimia 34 ya madai yote ya Sh 127.6 bilioni yaliyohakikiwa yameonekana ni sahihi na kulipwa bila

marekebisho.

Amesema madai yanayostahili kulipwa yanajumuisha Sh16.25 bilioni kwa

walimu 15,919 na Sh27.15 bilioni kwa watumishi wasiokuwa walimu 11,470

 

Amesema kwa kuwaondoa kwenye mfumo wa malipo ya mishahara, watumishi hewa, vyeti feki na wasiokuwa na sifa na uhakiki kwa madai ya malimbikizo ya mishahara uliofanyika limeweza kuokoa jumla ya Sh84.22

bilioni ambazo ni sawa na asilimia 66 ya malimbikizo ya awali.

“Serikali itaendelewa kulipa madai ya watumishi kadri yanavyojitokeza

ili kuondokana na malimbikizo ya aina hii ambayo yanaweza kuisababishia Serikali hasara kwa kulipa madai yasiyostahili,”alisema.