Serikali ya Tanzania yakataa wachunguzi wa nje kutekwa kwa Mo Dewji

Muktasari:

Naibu Waziri wa Mambo  ya Ndani Hamad Masauni amesema Serikali haiwezi kuruhusu vyombo vya ulinzi na usalama kutoka nje ya nchi kuchunguza tukio la kutekwa mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’

 


Zanzibar. Naibu Waziri wa Mambo  ya Ndani,  Hamad Masauni amesema Serikali haiwezi kuruhusu vyombo vya ulinzi na usalama kutoka nje ya nchi kuchunguza tukio la kutekwa mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’.

Masauni ametoa kauli hiyo leo Jumanne Oktoba 16, 2018 katika mkutano wake na waandishi wa habari.

Amesema ana amini polisi kuna wataalam wanaoijua kazi yao, wanaifanya kwa kuzingatia maadili.

“Kuna haja gani kuleta vyombo vya nje wakati tuna jeshi bora na lenye uelewa mkubwa licha ya kukabiliwa na changamoto za hapa na pale,” amesema.

Amesema  polisi hawajashindwa kuchunguza jambo hilo na lipo ndani ya uwezo wao.

Alipoulizwa kuhusu familia ya Mo Dewji kutangaza dau la Sh1bilioni kwa yeyote atakayetoa taarifa zitakazofanikisha kupatikana kwa mfanyabiashara huyo, Masuani amesema hawezi kulizungumzia suala hilo kwa kuwa si msemaji wa familia.

Hata hivyo, amesema wananchi wana nafasi ya kutoa taarifa kwa polisi  ili waweze kufanya kazi hiyo kwa haraka.