Serikali ya Tanzania yapokea gawio la Sh717.6 bilioni

Rais John Magufuli akimkabidhi cheti Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA), Jonas Kilimbe (kushoto) kutokana na mamlaka hiyo kuvuka kiwango cha gawio lake kwa serikali kwa mwaka wa fedha 2017/18 kutoka shilingi bilioni 13.2 hadi bilioni 22.3 , wakati wa wakati wa hafla ya makabidhiano iliyofanyika jijini Dar es Salaam jana. Kulia ni Waziri wa Fedha na Mipango, Philip Mpango. Picha na Ericky Boniphace


Muktasari:

Hazina imetoa ilani kwa wawekezaji tisa kuonyesha nia ya Serikali kuvitwaa viwanda


Dar es Salaam. Serikali imepokea gawio la Sh717.56 bilioni kutoka kwa kampuni, taasisi na mashirika ya umma kwa ajili ya mwaka 2018.

Akizungumza katika hafla ya kupokea gawio hilo leo Julai 23, 2018 jijini Dar es Salaam, Msajili wa Hazina, Athumani Mbutuka amesema gawio hilo ni kutoka kwa kampuni, taasisi na mashirika ya umma 43 kati ya 90 ambayo yanastahili kutoa gawio.

Mbutuka amesema changamoto iliyopo ni kuwa kuna baadhi ya kampuni zisizozingatia ubia baina yao na Serikali. Amesema zipo ambazo hutangaza kutoa gawio kwa wanahisa lakini hushindwa kuwasilisha serikalini.

Msajili amesema viwanda vingi vimekuwa vikisuasua akieleza kati ya 51 vilivyofungwa 12 vilikiuka masharti ya mkataba na wawekezaji wake hawakuonyesha nia ya kuviendeleza.

Amesema Hazina imetoa ilani kwa wawekezaji tisa kuonyesha nia ya Serikali kuvitwaa viwanda na kuviendeleza.

“Ubinafsishaji ulikuwa na nia ya kuongeza tija na isitafsiriwe kama tunafanya utaifishaji, tutavichukua, tutatangaza na kuwapa wawekezaji wengine ili kutimiza shabaha tuliyojiwekea,” amesema.

Amesema viwanda vitatu vimerejeshwa serikalini na wawekezaji wengine wamepewa.