Serikali ya Tanzania yasema watu 75 wametekwa kwa miaka mitatu

Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola 

Muktasari:

Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amesema hali ya usalama nchini imeendelea kuimarika licha ya matukio machache ya utekaji yanayoendelea.


Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amesema watu wapatao 75 wametekwa katika miaka mitatu.

Kauli ya Lugola imekuja ikiwa zimepita siku tatu tangu alipotekwa mfanyabiashara bilionea Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ huku akisema bado uchunguzi unaendelea.

Akizungumza leo Oktoba 13, 2018 na waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam,  Lugola amesema amefanya kikao na Mkuu wa Polisi nchini na kutafakari hali ya uhalifu nchini.

Amesema licha ya juhudi za polisi nchini, mwaka 2016 kulikuwa na matukio ya watu 9 kutekwa lakini watano walipatikana wakiwa hai kwa ushirikiano na wananchi.

"Watu wanne hawakupatikana, katika kipindi hicho watuhumiwa sita walikamatwa; watano walifikishwa mahakamani na mmoja aliuawa na wananchi," amesema Lugola.

Amesema mwaka 2017, watu 27 walitekwa na polisi walifanikiwa kuwapata 22 wakiwa hai na wawili wakiwa wamekufa, huku watatu hawakupatikana.

" Januari hadi Oktoba 11, 2018, watu 21 walitekwa ambapo kati yao 17 walipatikana wakiwa hai na wanne hawakupatikana hadi sasa. Watuhumiwa 10 walikamatwa na kufikishwa mahakamani," amesema.

Kuhusu utekaji wa watoto, Lugola amesema tangu mwaka 2016 ni watoto 18; kiume sita na wakike 12.

Soma zaidi:

"Watoto 15 walipatikana wakiwa hai, wawili walikutwa wamekufa na mmoja hajapatikana," amesema Lugola.

Ametaja sababu za utekaji huo kuwa ni za kisiasa, kiuchumi, kulipiza visasi, wivu wa mapenzi na ushirikina.