Serikali yaagiza mabasi mapya 165 ya mwendokasi

Muktasari:

Tayari imeshatangaza zabuni ya kununua mabasi hayo na mwezi Desemba, mwaka huu itasaini mkataba na mzabuni.

Dar es Salaam. Serikali imeanza mchakato wa kuagiza mabasi mapya 165 ya mwendokasi yatakayotoa huduma za usafiri kwa wakazi Dar es Salaam kwenye maeneo yasiyo na huduma hiyo.

Tayari imeshatangaza zabuni ya kununua mabasi hayo na mwezi Desemba, mwaka huu itasaini mkataba na mzabuni.

Mtendaji Mkuu wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Kasi (Dart), Ronald Rwakatare amewaeleza wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa waliotembelea mradi huo kuwa wanatarajia mabasi hayo yataanza kazi Aprili mwakani.

“Mabasi haya yatahudumia maeneo ya Morocco, Tegeta, Masaki, Makumbusho na mengine yasiyofikiwa, wakati tukiendelea na ujenzi wa awamu ya pili ya mradi huo,” amesema.