Serikali yaainisha changamoto Tanzania ya Viwanda

Muktasari:

  • Wizara ya Viwanda imesema Serikali pekee haiwezi kutekeleza mpango wa kufikia uchumi wa kati bila kushirikisha sekta binafsi.

Dar es Salaam. Serikali imesema inatambua umuhimu wa kutatua changamoto zilizopo katika kutekeleza mpango wa kuwa nchi ya viwanda yenye uchumi  wa kati ifikapo mwaka 2025.

Imesema itafanya hivyo kwa kushirikiana na sekta binafsi ambayo ni muhimu katika kufanikisha mpango huo, unaotarajiwa kuondoa wananchi na Taifa kwenye kundi la masikini.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk Adelhelm Meru amesema hayo leo Ijumaa alipokutana na Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI) katika kutathmini mchango wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kufanikisha mpango huo.

"Uwapo wa mamlaka nyingi za usimamizi wa uwekezaji na biashara na kucheleweshwa kwa marejesho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ni miongoni mwa changamoto zilizopo ambazo Serikali itazishughulikia ili kuwa na viwanda vingi,” amesema Meru.

Kwa kutambua unyeti wa mpango huo, Dk Meru amesema Serikali pekee haiwezi kuufanikisha, hivyo kuhitaji ushiriki wa sekta binafsi inayopaswa kuzalisha bidhaa zenye ubora wa kukidhi viwango vya masoko ya nje ili kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka mataifa mengine.

Mwenyekiti wa CTI, Dk Samwel Nyantahe amesema wafanyabiashara na wawekezaji wote wanafahamu wajibu wa kulipa kodi na kwamba, Serikali inawajibika kuweka mazingira mazuri.

"Sera na usimamizi wa kodi ni mambo muhimu sana kufanikisha Tanzania ya viwanda. Hoja ya kuzingatiwa ni namna ya kulipa kodi na jinsi tunavyohudumiwa na mamlaka husika," amesema Dk Nyantahe.

Kamishina wa TRA, Charles Kichere amesema mamlaka inawajibika kuwasaidia wazalishaji wa ndani kwa kuweka mazingira mazuri ya kodi na biashara.

Mkurugenzi wa Sekta Binafsi (TPSF), Godfrey Simbeye amesema wanachohitaji wawekezaji ni sera nzuri ya uchumi na uwepo wa wataalamu wa kodi wa kutosha katika Wizara ya Fedha na Mipango ili kusimamia sera hiyo.