Serikali yabanwa itekeleze ahadi

Muktasari:

  • Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakulima hao walisema wakati wanaanza kuendesha kilimo cha mkonge walitarajia kupata mabadiliko makubwa yenye tija, lakini ukosefu wa mitaji umekuwa kikwazo kwao kutokufikia malengo.
  • Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima wa Mkonge Tarafa ya Magoma, Abdi Shekigenda alisema ukosefu wa hati miliki umechangia kuzorotesha maendeleo yao hususan katika ukuaji wa sekta ya kilimo.

Korogwe. Wakulima wa mkonge wa shamba la Magoma wilayani hapa, wameiomba Serikali kutekeleza ahadi yake ya kuwapatia hati miliki ili waweze kukopa mikopo kwenye taasisi za fedha na kuendesha kilimo chenye tija.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakulima hao walisema wakati wanaanza kuendesha kilimo cha mkonge walitarajia kupata mabadiliko makubwa yenye tija, lakini ukosefu wa mitaji umekuwa kikwazo kwao kutokufikia malengo.

Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima wa Mkonge Tarafa ya Magoma, Abdi Shekigenda alisema ukosefu wa hati miliki umechangia kuzorotesha maendeleo yao hususan katika ukuaji wa sekta ya kilimo.

Shekigenda alisema imekuwa vigumu kwa wakulima kunufaika na fursa zilizopo asasi za fedha.

Alisisitiza kuwa hati miliki kwao ni muhimu kwa kuwa zitawasaidia kukopa kwenye taasisi za fedha na kununua vitendea kazi kama matrekta badala ya kuendelea kulima kwa kutumia jembe la mkono.

Kutokana na hali hiyo, Shekigenda alisema kwamba wengi wao wanashindwa kujikwamua na umaskini kwa kutumia jembe la mkono kwa muda mrefu na kushindwa kulima sehemu kubwa.

Mwenyekiti huyo alieleza kuwa licha ya changamoto walizonazo, wanashukuru zao la mkonge kwa kukuza uchumi wao, kusomesha watoto, kupata vyombo vya usafiri na kujenga nyumba bora za kuishi wao kama wakulima.

Katibu wa Chama cha Wakulima wa Mkonge, Athumani Kaoneka aliitaja changamoto nyingine inayowakabili ni wizi wa nyaya za umeme katika maeneo yao.