Mwakilishi ahoji mapato yaliyokusanywa na TRA, ZRB

Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar, Dk Khalid Salum Mohamed

Muktasari:

Waziri wa Fedha amesema ana imani lengo la kukusanya Sh675.8 bilioni katika kipindi cha mwaka 2017/18 litafikiwa.

Zanzibar. Sh265.99 bilioni sawa na asilimia 98.4 zimekusanywa katika kipindi cha miezi mitano ya kwanza ya ukusanyaji wa mapato ya Serikali kazi iliyofanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB).

Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar, Dk Khalid Salum Mohamed amesema hayo katika kikao cha Baraza la Wawakilishi  kinachofanyika Chukwani nje kidogo ya Mji wa Zanzibar alipojibu swali la mwakilishi wa Kiwani, Mussa Foum Mussa aliyehoji mamlaka hizo za mapato zimekusanya kiasi gani.

Waziri alisema jana Jumatatu Desemba 11,2017 kuwa mamlaka hizo zilikadiriwa kukusanya Sh270.3 bilioni kwa kipindi cha miezi mitano kuanzia Julai,2017 hadi Novemba 2017.

Dk Mohamed amesema Sh154.6 bilioni  zimekusanywa na ZRB sawa na asilimia 96.7 kiwango ambacho ni pungufu kulinganisha na makadirio ya Sh159.8 bilioni katika kipindi hicho.

Amesema mapato hayo yanahusisha makusanyo ya kodi ya Sh136.23 bilioni na Sh18.57 bilioni ni mapato yasiyo ya kodi.

Waziri amesema TRA imekusanya Sh102.44 bilioni sawa na asilimia 100.7 ya makadirio ya kukusanya Sh101.7 bilioni.

Amesema mapato yatokanayo na mshahara (Paye) yamefikia Sh8.75 bilioni sawa na asilimia 100.

Dk Mohamed amesema hatua hiyo imefikiwa baada ya kuwepo kwa mikakati imara kwa taasisi hizo kuhusu ukusanyaji wa fedha za Serikali kupitia wafanyabiashara na vyanzo vingine vya mapato.

“Ni kawaida yetu mfanyakazi anapofanya vizuri kumpatia pongezi lakini kwa taasisi hizo tayari tumeanza nazo kwa kuwapa bonasi kwa kuthamini jitihada zao, hatua hii tunaona ni nzuri na tunaahidi kuiendeleza ili kuona watendaji hao wanaongeza nguvu katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali,” amesema.

Amesema Serikali imeingia mkataba kati ya ZRB na kampuni kutoka nchini Singapore kwa ajili ya kuwapatia mafunzo watendaji na wafanyakazi wa mamlaka hiyo ya utekelezaji wa kazi zao.

Amesema kiwango cha makusanyo kinatia moyo wa mamlaka hizo kufikia lengo la kukusanya Sh675.8 bilioni katika kipindi cha mwaka 2017/18.