Serikali yakiri ukeketaji bado ni ‘pasua kichwa’

Wanawake Jamii ya Kimasai wakimpigia makofi, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto, Faustine Ndugulile wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Kibirashi Wilaya ya Kilindi kwenye sherehe za maadhimisho ya kupinga ukeketaji Duniani. Picha na Rajabu Athumani.

Muktasari:

Naibu waziri aanika madhara na namna jamii inavyopaswa kupambana na tatizo hilo

Kilindi. Serikali imekiri kuwa tatizo la ukeketaji nchini bado linaisumbua, huku ikitaja mikoa mitano ambayo ni kinara kwa vitendo hivyo.

Vilevile imesema katika maeneo hayo kati ya wanawake 10, mmoja ni lazima anakuwa amekeketwa na kufanya kuwa na waathirika wengi zaidi wa vitendo hivyo.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Faustine Ndugulile alisema hayo jana akisisitiza kuwapo kwa madhara mengi kwa wanawake wanaokeketwa, hivyo Serikali kwa kushirikiana na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali itaendelea kutoa elimu.

Alisema wazazi na watu wanaofanya shughuli za ukeketaji wanatakiwa kuacha kwa kuwa wanawaathiri kiafya watoto wao, hasa wanapofikia umri wa kujifungua pamoja na kisaikolojia kwa wale wanaokuwa shule. Naibu waziri huyo aliongeza kuwa kwa wale ambao wanasoma ukeketaji unazorotesha hata maendeleo yao shule.

Alisema katika baadhi ya maeneo watoto huzuiwa kwenda shule kwa ajili ya kufanyiwa vitendo hivyo.

“Mwanamke mmoja kati ya wanawake 10 amekeketwa na mikoa inayoongozwa (na viwango kwa asilimia katika mabano) ni Manyara (58), Dodoma (47), Arusha (41), Mara (32) na Singida (31). “Hizi takwimu ndugu zangu ni kubwa sana na madhara yake kwa watoto pia ni pamoja na kupoteza damu,” alisema Ndugulile.

Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Amref Health Africa, Florence Temu alisema kuanzia mwaka 2014 hadi sasa katika Wilaya ya Handeni na Kilindi wamewaokoa watoto 3,070 kukeketwa ambapo 880 wanatoka Handeni na 2,014 wanatokea Kilindi.

Alisema tatizo la ukeketaji lipo duniani kote ambapo katika nchi 30 wasichana milioni 200 wanakeketwa kwa takwimu za mwaka 2015.

Temu aliitaka Serikali kuongeza nguvu kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali kupinga vitendo hivyo.

Mkuu wa Wilaya ya Kilindi, Sauda Mtondoo alitoa shukrani kwa mashirika yanayotoa elimu ya kupinga ukeketaji na kuwataka wananchi kuzingatia elimu inayotolewa, huku akizitaka sekta nyingine kuongeza nguvu kupinga suala hilo.

Alisema jamii inatakiwa kuwapeleka watoto shule na kuachana na mila ambazo zimekuwa na madhara hasa wale wa kike ambao ndio wasimamizi wa familia kwa siku za usoni watakapokuwa wazazi.

Kiongozi wa mila kutoka jamii ya Wamasai, Laigwanani William Tangano alisema wameshaelewa madhara ya vitendo vya ukeketaji na wamekubali kuacha.

Tangano alisema kufuatia uamuzi huo, vijana wa rika la kuoa wa jamii hiyo (morani) wamekubali kuoa wanawake ambao hawajakeketwa.

Hata hivyo, aliiomba Serikali kuendelea kutoa elimu kwa wananchi hususan wa jamii anayotoka ili wasifikirie tena kurejea katika utamaduni huo aliodai umepitwa na wakati. Tangano aliiomba Serikali kuchukua hatua za kisheria kwa watu ambao wanaendeleza ukeketaji kwa kuwa bila kufanya hivyo wapo ambao wataendelea.