Serikali yakusanya Sh32 bilioni kodi ya majengo nchini

Dar es Salaam.  Baada ya mshikemshike wa ulipaji wa kodi ya majengo uliosababisha Serikali iongeze siku 15, jumla ya Sh32.5 bilioni zimekusanywa.

Kiasi hicho cha kodi ya jengo kimekusanywa katika mwaka wa fedha 2016/17 katika manispaa, miji na majiji 30 nchini.

 Mwisho wa kulipa kodi ya majengo ilikuwa Juni 30, lakini Serikali iliongeza muda hadi Julai 15 na sasa imeongeza tena hadi Julai 30.

Misururu ya walipakodi ilionekana katika ofisi za Mamlaka ya Mapato(TRA) na kusababisha mitandao kushindwa kufanya kazi kwa wakati.

Akizungumza na waandishi wa habari jana,  Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema makusanyo hayo ni sawa na asilimia 56 ya lengo lililowekwa kwaka uliopita wa fedha la kukusanya Sh58 bilioni.

Alisema, halmashauri zilikusanya Sh28.3 bilioni wakati TRA imekusanya Sh32.5 bilioni tangu ianze kukusanya kodi hiyo Oktoba mwaka jana.

“Mapato hayo yanatarajiwa kuongezeka kutokana na mwitikio mkubwa wa wananchi kulipa kodi ya majengo,” alisema Mpango.

Waziri huyo aliwapongeza wananchi kwa mwitikio wao, akisema  wameonyesha uzalendo wa kweli na ndio maana Serikali imeamua kuongeza muda wa kulipa kodi hiyo bila adhabu hadi Julai 30 mwaka huu.

Katika hatua nyingine, Dk Mpango amewapongeza wamiliki wa vituo vya mafuta waliotii  maagizo ya Serikali, kwa kufunga mashine za kielektroniki za risiti, akitaja vituo vya Puma na Total kuwa  vimeonyesha mfano wa kuigwa.

Aliwaonya wamiliki wengine  wa vituo vya mafuta ambao hawatafunga mashine hizo hizo zinazounganishwa katika kampu za mafuta kuwa iwapo hawatatii agizo la kufanya hivyo ndani ya siku 14 zilizotolewa na  Rais John Pombe Magufuli, watachukuliwa hatua kali.

“Baada ya muda huo, mtu asije kuilaumu Serikali itakapoanza kuchukua hatua kali za kisheria,” alisema Dk Mpango.

Kadhalika, aliwataka wenye maduka ya vifaa vya ujenzi, vileo na maduka makubwa kutumia mashine hizo kikamilifu na kutoa risiti kwa wateja wao.

 Pia aliwashauri wateja kudai risiti wanapofanya manunuzi.

Alipiga marufuku wafanyabiashara wanaosingizia mashine za EFDs kuwa mbovu na kuwaonyesha wateja wao karatasi kusingizia kuwa wameitaarifu TRA kuhusu ubovu wa mashine zao.

“TRA muhakikishe wafanyabiashara ambao mashine zitakuwa hazitumiki ndani ya saa 48 kwa kisingizio cha kuharibika, zifungiwe na wamiliki watozwe faini,” alisema.