Serikali yalaani kushambuliwa wanahabari wakiwa kazini

Muktasari:

Mkurugenzi, Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbasi katika taarifa yake leo, amesema ifahamike kuwa uandishi wa habari ni taaluma adhimu inayopaswa kuheshimiwa, kuenziwa, kulindwa na kutoingizwa katika migogoro ya pande zinazofarakana katika jamii.

Dar es Salaam. Serikali imelaani kuumizwa wanahabari walioalikwa kuhudhuria mkutano wa Chama cha Wananchi (CUF) Jumamosi iliyopita.

Mkurugenzi, Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbasi katika taarifa yake leo, amesema ifahamike kuwa uandishi wa habari ni taaluma adhimu inayopaswa kuheshimiwa, kuenziwa, kulindwa na kutoingizwa katika migogoro ya pande zinazofarakana katika jamii.

“Serikali imepokea kwa masikitiko taarifa za kushambuliwa na kujeruhiwa baadhi ya waandishi wa habari katika mvutano uliotokea juzi jijini Dar es Salaam kati ya wafuasi wa pande mbili zinazokinzana za CUF.

“Tumechukua muda kidogo kulifuatilia suala hili na kubaini licha ya baadhi yao kujeruhiwa na kuripoti polisi, wapo waandishi ambao vifaa vyao vya kazi pia vililengwa katika shambulizi hilo,” alisema Dk Abbasi.

Alisema kifungu cha 7 (1) (a) cha Sheria ya Huduma za Habari Na. 12 ya mwaka 2016 kinaainisha uhuru wa wanahabari katika kukusanya habari kwa muktadha wa kuwapo katika maeneo ya matukio kama hakuna sababu nyingine za kuzuiwa.

“Misingi ya uhuru huu wa kitaaluma pia imesisitizwa katika Ibara za 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 na 19 ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa wa mwaka 1966 ambao nchi yetu imeuridhia,” alisema.

Dk Abbasi alisema, “Kwa kuwa suala hili tayari limeripotiwa polisi, tunawaomba wadau wote wa habari na wanasiasa kwa sasa kutulia na kuviachia vyombo husika vilifanyie kazi ili hatua stahiki za kisheria zichukuliwe.”