Monday, January 15, 2018

Gazeti la Nipashe lajiadhibu

 

By Peter Elias, Mwananchi pelias@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Serikali imeridhia hatua zilizochukuliwa na uongozi wa kampuni ya IPP Media kumuomba radhi Rais John Magufuli na kulifungia gazeti la Nipashe Jumapili kwa muda wa miezi mitatu kutokana na kuchapisha habari ya uzushi na upotoshaji.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbas, leo Januari 15, 2018, gazeti hilo lilichapisha habari katika toleo namba 0579459 la Jumapili Januari 14, yenye kichwa cha habari “JPM akerwa wanaomtaka adumu urais kama Kagame.”

Dk Abbas amesema habari hiyo ilisheheni uzushi na upotoshaji na kwamba mwandishi aliihusisha isivyo halali Serikali ya Rwanda katika taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasilisno ya Rais (Ikulu) juu ya Rais Magufuli kusisitiza kwamba hana nia ya kubadili Katiba ili kujiongeza muda wa kukaa madarakani.

“Kwa makosa haya na hatua zilizochukuliwa haraka na wahusika, tunatumia fursa hii kuwapongeza wamiliki na wahariri wa Nipashe Jumapili na IPP Media kwa wao wenyewe kujitathmini, kujikosoa na kujisahihisha,” amesema Dk Abbas.

Amesema pamoja na hatua hizo ambazo IPP Media wamezichukua na Serikali kuzibariki, Rais Magufuli pia amemjulisha kwamba amepokea radhi zao.

Dk Abbas ametoa wito kwa wamiliki wa vyombo vya habari na waandishi wa habari kuzingatia misingi na weledi wa kitaaluma.

 

 

-->