Serikali yangilia kati mgogoro

Muktasari:

  • Wananchi wa kijiji hicho wanailalamikia TFS kubadilisha mpaka kati ya kijiji na Hifadhi ya Msitu wa Sakaya, hivyo kuwasababishia wakose maeneo ya kuchungia mifugo na kilimo.

Mwanza. Serikali imesema itatumia njia rahisi za kisheria kutatua mgogoro wa ardhi  baina ya wananchi wa Kijiji cha Bugatu, Kata ya Nhaya wilayani Magu mkoani Mwanza na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), uliodumu kwa zaidi ya miaka 20.

Wananchi wa kijiji hicho wanailalamikia TFS kubadilisha mpaka kati ya kijiji na Hifadhi ya Msitu wa Sakaya, hivyo kuwasababishia wakose maeneo ya kuchungia mifugo na kilimo.

Hifadhi ya Msitu wa Sakaya ilianza mwaka 1985, lakini  kumekuwa na mvutano baina ya Serikali na wanakijiji tangu mwaka 1995 na mwaka 2012 wananchi wanaodaiwa kuvamia eneo hilo nyumba zao zilichomwa moto na kutakiwa kuondoka.

Akizungumza na wananchi hao mwishoni mwa wiki iliyopita alipowatembelea kujua kiini cha mgogoro huo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Ramo Makani alisema  Serikali haitaki migogoro isiyo ya lazima baina yake na wananchi na kutaka pande zote kuheshimu na kusimamia sheria.