Washirika wa Zuma, mtoto wake wasakwa China, India

Muktasari:

Watuhumiwa wengine wanane walikamatwa wiki iliyopita na wamefikishwa mahakamani.

 


Johannesburg, Afrika Kusini. Serikali imepanua eneo la kufanyia uchunguzi wa rushwa dhidi ya washirika wa rais wa zamani Jacob Zuma hadi nchi nyingine za India, China na Dubai, Waziri wa wa Mambo ya Ndani alisema Jumapili.

Waziri Fikile Mbalula alitoa maelezo hayo siku kadhaa baada ya Afrika Kusini kutoa hati ya kukamatwa kwa mmoja wa ndugu wa familia ya wafanyabiashara ya Gupta, washirika wa karibu wa Zuma aliyegubikwa na kashfa hadi akalazimishwa kujiuzulu Jumatano.

Mbalula aliliambia Shirika la Utangazaji la SABC kwamba Ajay Gupta na watu wengine wanne ambao wanatafutwa kuhusiana na kesi hiyo walikuwa nje ya nchi.

Japokuwa hakukuwa na ishara zozote kwamba walikimbia nchi wakiogopa kukamatwa, Mbalula aliapa kwamba "watasakwa" kokote waliko kupitia Polisi wa Kimataifa, Interpol, huku kukiwa na uwezekano wa kurejeshwa ili kukabiliana na kesi nchini Afrika Kusini.

 

Alisema wawili kati ya watuhumiwa ni wa asili ya India na mwingine mmoja ni Mchina. Wote wanafikiriwa kuwa wako India, China au Dubai.

"Tunafanya kazi kupitia Interpol, tunatumia njia ya ushirikiano, ikiwa unakataa utarejeshwa. Njia zote muhimu zitatumika ili kuhakikisha kuwa watu hawa wanakamatwa na kuletwa nchini," alisema Mbalula.

Waziri alikataa kuwataja watuhumiwa isipokuwa Ajay Gupta ambaye wiki iliyopita polisi walitangaza kuwa amekimbia.

Ripoti za vyombo vya habari zinaonyesha kuwa mwana wa Zuma, Duduzane Zuma, mshirika wa kibiashara wa akina Gupta, pia ni kati ya wale wanaotafutwa, na wengine walidhani kwamba anaweza kuwa Dubai.

Hata hivyo, waziri alikataa kueleza ikiwa Duduzane Zuma yuko kwenye orodha ya watu wanaotafutwa na polisi. "Kamatakamata itawakumba wengi zaidi ... hatumtafuti mchawi," aliongeza.

"Haijalishi, kama wewe ni mwanasiasa ... hakuna ng'ombe watakatifu, hakuna watu wasiokamatika."

Kati ya wanaosakwa, watu 13 wanakabiliwa na mashtaka yanayohusu madai kwamba mamilioni ya dola za Marekani ambayo yalitengwa kwa ajili ya wafugaji maskini wa ng’ombe wa maziwa yaliingia kwenye mifuko ya akina Gupta. Watuhumiwa wengine wanane walikamatwa wiki iliyopita na wamefikishwa mahakamani.

Katika hotuba yake ya kwanza kwa taifa baada ya kushika mamlaka siku ya Ijumaa, Rais mpya wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa aliapa kupambana na rushwa shutuma ambazo alikuwa akitupiwa mtangulizi wake Zuma.