Serikali yazungumzia miradi ya maji Makete

Muktasari:

Naibu Waziri wa nchi ofisi ya Rais Tamisemi, Joseph Kandege amesema Serikali imeanza ukarabati wa mradi huo ambao bomba jipya la umbali wa kilomita 4 limelazwa.


Dodoma. Serikali imesema mradi wa maji wa Bulongwa na Magoma ulijengwa mwaka 1984 na kuhudumia vijiji 14 haukidhi mahitaji ya sasa kutokana na uchakavu wa miundombinu yake.

Naibu Waziri wa nchi ofisi ya Rais Tamisemi, Joseph Kandege amesema Serikali imeanza ukarabati wa mradi huo ambao bomba jipya la umbali wa kilomita 4 limelazwa.

Ametoa maelezo hayo bungeni leo Februari 9, 2018 wakati akijibu swali la msingi la mbunge wa Makete (CCM), Profesa Norman Sigalla (CCM) aliyetaka kujua Serikali itakamilisha lini ujenzi wa mradi wa maji wa tarafa ya Matamba ili wananchi waondokane na adha ya kufuata maji mbali.

Mbunge huyo pia amehoji ni lini Serikali itakamilisha mradi wa maji wa tarafa ya Bulongwa na Magoma ili kata za Bulongwa, Kipagalo na Luwumbu ziweze kupata maji.

Katika majibu yake, Kandege amesema mchakato wa kumpata mkandarasi atakayetekeleza awamu ya pili ya ukarabati huo katika bomba la kilomita mbili utakamilika Juni 30, 2018.