Serikali yatakiwa kuendelea kutatua kero za muungano

Muktasari:

Kamati nyingine zilizowasilisha taarifa zake jana ni  Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa na Kamati ya Sheria Ndogo.

 


Dodoma. Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria imeiagiza Serikali kuendelea kutatua kero za muungano na kuhakikisha wananchi wa

pande zote mbili wanatumia na kufaidika na fursa mbalimbali zinazotokana na muungano huo.

Agizo hilo limetolewa na kamati hiyo jana Februari 8, 2018 ilipowasilisha taarifa za utekelezaji wa shughuli zake.

Kamati nyingine zilizowasilisha taarifa zake jana ni  Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa na Kamati ya Sheria Ndogo.

Mwenyekiti wa kamati ya Katiba na Sheria, Mohamed Mchengerwa amesema kumekuwa na kero mbalimbali tangu kuasisiwa kwa

Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, mwaka 1964.

Amesema jitihada mbalimbali zimechukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kutatua kero mbalimbali.

“Kamati inashauri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) kupitia Tume ya pamoja ya kutatua kero za muungano kuendelea kutatua kero mbalimbali na kuhakikisha wananchi wa pande zote mbili wanatumia na kufaidika na muungano huo,”amesema,

“Zipo kero ambazo Ofisi ya Makamu wa Rais inatakiwa kuendelea kuzitatua kupitia Kamati Maalum ili kuendelea kudumisha Muungano.”

Amezitaja kero hizo kuwa ni ajira kwa watumishi wa Zanzibar katika taasisi za Muungano, ushirikiano  wa Zanzibar na taasisi za nje pamoja na uwezo wa Zanzibar kukopa ndani na nje ya nchi.

Nyingine ni ushiriki wa Zanzibar katika jumuiya ya Afrika Mashariki, mgawanyo wa mapato ya kodi na msaada, wafanyabiashara wa Zanzibar kuendelea kutozwa kodi mara mbili, utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asili na usajili wa vyombo vya moto.

“Kero hizi zinaendelea kutatuliwa na Serikali zote mbili na jitihada kubwa zimefanyika na Serikali ya Muungano kuhakikisha kwamba kero hizi

zinapungua,”alisema.

Kuhusu mrundikano wa kesi, Mchengerwa amesema, “Mrundikano wa kesi mahakamani

kuanzia za mwanzo hadi mahakama ya Rufaa bado ni kubwa sana.”

“Mfano Mahakama ya Rufaa ya Tanzania kwa muda wa miaka sita mfululizo idadi ya majaji imebakia kuwa ni 15 lakini idadi ya mashauri imekuwa ikiongezeka kila mwaka.”

Ametaja idadi ya mashauri na mwaka 2012 mashauri 2466, mwaka 2013 (2629), 2014 (2916), 2015 (3,244), 2016 (3,975) na mwaka 2017 mashauri 4,439.

Athari za uhakiki wa watumishi

Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa imeagiza Serikali kuongeza juhudi ili kuongeza idadi ya wataalam wa afya katika ngazi zote kukabiliana na upungufu unaotokana na mazoezi ya uhakiki wa

watumishi wa umma.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Jasson Rweikiza amesema upungufu huo umetokana na mishahara hewa na kuondoa watumishi walioajiriwa kwa

vyeti vya darasa la saba baada ya mwaka 2004.

“Uhakiki huo umeathiri sekta mbalimbali kutokana na kupoteza watumishi wengi kwa kuondolewa kazini. Miongoni mwa sekta hizo ni afya kwenye

sekretarieti za mikoa na serikali za mitaa,”amesema.

Alisema sekta hiyo ilipoteza watumishi 3310 wa kada mbalimbali za afya kutokana na uhakiki wa vyeti pekee na hivyo kuongeza upungufu

kutoka asilimia 51 iliyokuwepo kabla ya uhakiki hadi asilimia 54.4 mara baada ya uhakiki.

“Upungufu huo wa wataalam katika sekta hiyo ulifikia watumishi 57.8. Kamati imetambua na kupongeza juhudi za Serikali katika kukabiliana na

upungufu huo ikiwa ni pamoja na kutoa kibali na kuajiri madaktari 206 waliotakiwa kwenda nchini Kenya na kuwatawanya katika mikoa na mamlaka

za Serikali za Mitaa Mei mwaka jana,”amesema.

Hata hivyo, amesema kwa kuzingatia juhudi za Serikali za Mitaa ni wazi kwamba wananchi bado wanapata shida katika kupata huduma za afya na

kwamba zinahitajika juhudi zaidi za makusudi ili kuongeza idadi ya wataalam wa afya katika ngazi hizo.