Wazee wataka utungwaji sheria kuharakishwa

Muktasari:

Wazee wengi wanaishi katika hali duni isiyo na uhakika wa kipato.

Dar es Salaam. Jukwaa la Wazee Tanzania limeiomba Serikali kuharakisha utungaji sheria ili kulinda haki zao.

Mkurugenzi wa asasi ya wazee mkoani Morogoro, ambaye ni mwakilishi wa jukwaa hilo, Samson Msemembo amesema wazee wanashindwa kutatua changamoto zinazowakabili kwa kukosa sheria inayoongoza upatikanaji wa haki zao.

Amesema wazee wanatambulika katika kundi la wasiojiweza lakini kumekuwa na matukio ya kikatili na kukosekana kwa haki za msingi na hasa katika sekta ya afya.

Msemembo akizungumza na MCL Digital amesema licha ya maazimio ya haki za binadamu kuzuia kutobagua watu kutokana na umri lakini utekelezaji ni ndogo.

“Wazee wengi wanaishi katika hali duni isiyo na uhakika wa kipato, wanaopata pensheni ni asilimia nne ya wazee wote na takwimu zinaonyesha familia zinazoongozwa na wazee umasikini upo juu kwa asilimia 24.4 zaidi ya wastani wa umasikini wa nchi,” amesema Msemembo.

Hata hivyo, ameishukuru Serikali kwa kuboresha sekta ya afya na kuwapa kipaumbele wazee.

“Tunaipongeza Serikali kwa kuboresha upatikanaji wa huduma za afya ingawa bado tunapata changamoto katika upatikanaji wa dawa na hasa katika zahanati,” amesema mjumbe wa asasi hiyo, Wilson Karwesa.

Amesema wanakabiliwa na changamoto ya umasikini wa kipato, unyanyasaji na mauaji ya wazee hasa katika mikoa ya kanda ya ziwa. Pia, kukosa wawakilishi katika vyombo vya uamuzi.

Karwesa amesema wana imani kuwa sheria ya wazee itakapotungwa changamoto hizo zitapungua na huenda zikatoweka kabisa.