Serikali yatakiwa kuongeza thamani ya matikiti

Muktasari:

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana walisema wanalazimika kuwakopesha madalali matikiti na kulipwa baadaye, huku baadhi wakiwalipa kinyume na makubaliano.

Kibaha. Wakulima wa matikiti wilayani hapa mkoani Pwani wameishauri Serikali kuanzisha viwanda vya kusindika zao hilo ili kuliongezea thamani na kupata bei kubwa tofauti na ilivyo sasa.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana walisema wanalazimika kuwakopesha madalali matikiti na kulipwa baadaye, huku baadhi wakiwalipa kinyume na makubaliano.

Mkulima kijijini Mwendapole, Felician Bwemelo alisema: “Naiomba Serikali iangalie uwezekano wa kutusaidia wakulima, unavyoniona kilimo hiki nilianza tangu mwaka 1990 lakini sijapata maendeleo, nimekuwa nikidhulumiwa na madalali.”

Alisema wakati wa mavuno madalali hufika kwenye mashamba yao na kufanya maelewano ya bei kisha kuvuna na kuondoka, baada ya hapo hawarudi kufanya malipo.