Serikali yateketeza vifaranga 67,500 kutoka nje ya nchi

Muktasari:

Kauli hiyo ilitolewa bungeni na Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William Ole Nasha alipojibu swali la Mbunge wa Ukonga (Chadema), Waitara Mwita ambaye alitaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuzuia uingizaji mayai kutoka nje kwa sababu yanaharibu soko la ndani la bidhaa hiyo.

Dodoma. Serikali imeeleza kuwa vifaranga 67,500 kutoka nje ya nchi vilivyoingizwa nchini kinyume cha sheria kuanzia mwaka 2013 hadi 2017 viliteketezwa.

Kauli hiyo ilitolewa bungeni na Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William Ole Nasha alipojibu swali la Mbunge wa Ukonga (Chadema), Waitara Mwita ambaye alitaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuzuia uingizaji mayai kutoka nje kwa sababu yanaharibu soko la ndani la bidhaa hiyo.

Pia, alihoji Serikali ina mpango gani wa kusimamia malighafi ili chakula cha mifugo kiendane na bei ya mayai na kuku na kama ipo tayari kusimamia wananchi walipwe fidia kutoka kwa wawekezaji wanaoingiza vifaranga wasio na chanjo kutoka nje na kusababishia hasara.

Naibu Waziri, Ole Nasha alisema hakuna mwekezaji yeyote aliye pewa kibali cha kuingiza vifaranga au mayai nchini kwa ajili ya biashara.

Alisema kuanzia mwaka 2006 Serikali iliweka katazo la kuingiza kuku na mazao yake nchini ili kudhibiti ugonjwa hatari wa mafua ya ndege usiweze kuenea maeneo mengi na kuwapa hasara wakulima.

“Sheria ya Magonjwa ya Wanyama namba 17 ya mwaka 2003 na kanuni zake za mwaka 2007 na 2010 zinatumika kudhibiti na kukagua uingizaji katika maeneo ya mpakani, bandarini na viwanja vya ndege,” alisema.

Alisema Serikali inasimamia ubora wa malighafi na kusindika vyakula vya mifugo, kupitia sheria ya maeneo ya nyanda za malisho na rasilimali za vyakula vya wanyama namba 13 ya mwaka 2010.

Alitaja changamoto katika kusindika vyakula kuwa ni gharama kubwa ya viini lishe vya protini kutokana na matumizi ya maharage aina ya soya na kwamba Serikali inaendelea kuhamasisha uzalishaji wa soya hapa nchini.