Serikali yatoa Sh1.2 bilioni kutatua kero ya maji Monduli

Muktasari:

Aweso awataka wananchi Monduli kumchagua mgombea wa CCM kuzisimamia

Monduli. Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso amesema Serikali imetoa Sh1.2 bilioni kutatua tatizo la maji katika mji wa Monduli jijini Arusha na kuwataka wananchi kumchagua Julius Kalanga mgombea ubunge wa CCM kuzisimamia.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni katika uwanja wa Monduli mjini, Aweso alisema Serikali inazitambua kero za wananchi wa Monduli na tayari ilianza kuzifanyia kazi.

Alisema kazi ya Mbunge ni kuwatetea wananchi na Kalanga na kwamba alikwisha anza kazi hiyo na ndiyo sababu Serikali ilitoa fedha kwa wilaya hiyo lakini  alikuwa anakosa ushirikiano ambao sasa ataupata baada ya kujiunga na CCM.

Hata hivyo, Aweso alionya mtu yoyote ambaye atakula fedha hizo za maji kwani atazitapika mapema.

"Mimi ni mdogo lakini najiamini, ukizingua tunazinguana nakutimua. Sitakubali kutumbuliwa na Rais John Magufuli watu wakikosa maji" alisema Aweso.

Akizungumza katika mkutano huo, Kalanga aliishukuru serikali kwa kutambua kero za wananchi wa Monduli na kuanza kuzifanyia kazi.

Hata hivyo, aliomba Serikali kutazama upya gharama za kuunganisha maji zipunguwe kwani Sh400,000 ni kubwa.

"Wananchi wangu wanashida ya maji, lakini gharama ni kubwa tunaomba Naibu Waziri mkatusaidie hili, lakini pia kuna gharama za kuchimba msingi tunaomba kama wananchi wanaweza wafanye wao," alisema.

Meneja kampeni wa CCM Monduli, William Ole Nasha alisema chama hicho kitaendelea kupokea kero za wananchi na kuzifanyia kazi.

"Niliahidi kuwaleta mawaziri mbalimbali wamekuja na wamesikiliza kero na ambazo zinaweza kutatuliwa zimetatuliwa, kikubwa tunawaomba kumchagua Kalanga ili asimamie ahadi hizi" alisema.

Nasha alisema katika wilaya hiyo, alibaini kero ya shule kutosajiliwa licha ya wananchi kuzijenga lakini sasa tayari zimesajiliwa.