Serikali yatuma madaktari bingwa kuokoa maisha ya waliojeruhiwa kwa bomu

Muktasari:

  • Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Dk Revocatus Ndyekobora akizungumza na waandishi wa habari hospitalini hapo jana asubuhi, alisema timu ya madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera imewasili Ngara kusaidiana na wenzao kuwafanyia uchunguzi na kuwatibu majeruhi hao.

Ngara. Serikali imepeleka madaktari bingwa katika Hospitali ya Misheni ya Rulenge wilayani Ngara watakaoshiriki kuwatibu majeruhi 43 wa mlipuko wa bomu ulitokea katika Shule ya Msingi Kihinga.

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Dk Revocatus Ndyekobora akizungumza na waandishi wa habari hospitalini hapo jana asubuhi, alisema timu ya madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera imewasili Ngara kusaidiana na wenzao kuwafanyia uchunguzi na kuwatibu majeruhi hao.

“Watakaobainika kuhitaji huduma maalumu watahamishiwa hospitali zingine kulingana na taarifa ya madaktari,” alisema Dk Ndyekobora.

Alisema majeruhi hao pia wanahitaji uniti 50 za damu ili kuokoa maisha yao na kwamba, baadhi wamebainika kuwa na vipande vya vyuma vilivyotokana na mlipuko wa bomu.

“Tayari wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Mtakatifu Alfred Rulenge inayomilikiwa na Kanisa Katoliki Jimbo la Rulenge wamechangia uniti 46 za damu kusaidia wenzao,” alisema.

Mbali ya damu, majeruhi pia wanahitaji mashuka na mablanketi zaidi ya 50 kutokana na yaliyopo kutotosheleza mahitaji. Alisema baadhi wamelazimika kulala sakafuni kutokana na vitanda kujaa.

“Msaada wa chakula pia unahitajika kwa ajili ya majeruhi hawa ambao wametoka maeneo ya mbali kiasi cha kutowezesha wazazi, ndugu, jamaa na marafiki kuwaletea chakula,” alisema Dk Ndyekobora.

Usafiri kwa ajili ya kuwahamishia hospitali zingine pia ni miongoni mwa mahitaji ya dharura yanayohitajika kuokoa maisha ya majeruhi hao.

Katika hatua nyingine, mwanafunzi aliyeokota bomu la kutupa kwa mkono akidhani ni chuma chakavu kwa lengo la kwenda kuuza imebainika ni miongoni mwa watano waliokufa baada ya kulipuka.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Agustino Ollomi amemtaja mwanafunzi huyo kuwa ni Juliana Tarasisi (13).

Alisema jana kuwa, mwanafunzi huyo alilitunza bomu hilo kwenye begi lake la madaftari ili kwenda kuliuza kwa mnunuzi wa chuma chakavu wakati wa mapumziko.

Wanafunzi wengine waliopoteza maisha katika tukio hilo lililotokea jana ni Evart Theonas (12) Edson Bigilimana (12), Miburo Gabriel (12) na Tumsifu Ruvugo (8).

Wanafunzi 42 wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Kihinga na mwalimu wao wa darasa, Policalipo Clemency aliyekuwa darasani wakati wa tukio wamelazwa kwa matibabu katika Hospitali ya Misheni ya Rulenge.

Wakati huohuo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara, Aidan Bahama amepiga marufuku biashara ya vyuma chakavu katika maeneo ya shule akionya kuchukua hatua dhidi ya mwalimu mkuu na wakuu wa shule watakaobainika kuruhusu biashara hiyo.

Amri ya Bahama imetokana na uchunguzi wa awali wa polisi kubaini mwanafunzi mmoja aliokota bomu na kulihifadhi kwenye begi lake kwa lengo la kuliuza kama chuma chakavu.

Halmashauri kugharamia mazishi

Bahama alisema halmashauri imechukua dhamana ya kugharimia majeneza na shughuli za mazishi ya watoto watano waliokufa katika tukio hilo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Erick Nkilamachumu na mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Ngara, George Lubagola wameiomba Serikali kuimarisha ulinzi na ukaguzi kwa watu wanaingia nchini kutoka Burundi ili kudhibiti uingiaji holela wa silaha na mabomu ya kutupa kwa mkono.

Kijiji cha Kihinga ni miongoni mwa maeneo yanayopakana na nchi jirani za Burundi na Rwanda na kuna mwingiliano wa watu katika shughuli za kiuchumi na kijamii.