Serikali yawaangukia wafugaji kumaliza migogoro

Muktasari:

Akizungumza jijini hapa jana, katika ufunguzi wa warsha iliyowakutanisha watetezi wa haki za wafugaji nchini, Katibu Tawala Wilaya ya Arusha, David Mwakiposa alisema lengo ni kuwajengea uwezo waweze kuondoa migogoro.

Arusha. Serikali imewaomba viongozi wa Chama cha Wafugaji Tanzania na watetezi wa haki za wafugaji, kuhakikisha wanaondoa migogoro na wakulima ambayo imekuwa ikijitokeza na kurudisha maendeleo nyuma.

Akizungumza jijini hapa jana, katika ufunguzi wa warsha iliyowakutanisha watetezi wa haki za wafugaji nchini, Katibu Tawala Wilaya ya Arusha, David Mwakiposa alisema lengo ni kuwajengea uwezo waweze kuondoa migogoro.

“Serikali tunaomba watetezi wa haki za wafugaji kuangalia kwa uzito wa kipekee kuondoa migogoro ya wafugaji na wakulima, wahamasishe uanzishwaji wa viwanda vya kuchakata bidhaa za mifugo ili kumuunga mkono Rais John Magufuli katika sera ya viwanda,” alisema Mwakiposa.

Mwakiposa alisema sekta ya wafugaji na kilimo inaajiri zaidi ya asilimia 70 ya wananchi, ndiyo sekta pekee ambayo haihitaji elimu kubwa tofauti na ajira za viwandani na sehemu nyingine, hivyo ni muhimu kujengwa uwezo.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa alisema ni vizuri wakajengewa uwezo katika sera, sheria na mifumo ya utoaji haki katika Taifa na nje ya nchi ili waweze kutetea vizuri wafugaji.

“Tunaamini watetezi hawa wakifahamu vizuri sera na sheria wataweza kuangalia mifumo ya utoaji haki kama haitendeki, kwa wafugaji wataweza kutumia fursa hiyo kuwatetea vizuri,” alisema.

Katibu wa chama cha wafugaji nchini, Maghembe Makoye alisema Tanzania ina mifugo mingi hivyo ni muhimu wahusika wa sekta hiyo kujengewa uelewa na kujielekeza kuunda mabaraza ya usuluhishi ngazi za vijiji, kata, tarafa hadi wilaya ili kuhakikisha kundi hilo haligombani.

“Ni vizuri tukihamasishana kufuga kisasa ili kujiongezea tija katika uzalishaji wa bidhaa za wafugaji na kupata masoko ndani na nje ya nchi,” alisema.